Saturday, November 3, 2012

Vigogo wanaswa mtego wa fumanizi walipa mamilioni


UTAPELI wa aina yake, umeibuka mkoani Kilimanjaro ambapo kundi la matapeli hula njama na wanawake kuandaa mitego ya fumanizi na kujipatia mamilioni ya shilingi.
Uchunguzi wa kina wa Mwananchi Jumapili umebaini kuwa kundi hilo limekuwa likiwalenga wanaume walio katika ndoa na wenye uwezo wa kifedha, ambao baada ya kunaswa katika fumanizi hizo hupigwa picha zinazogeuzwa mradi.
Utapeli huo unawalenga wafanyabiashara, watu wenye nyadhifa kwenye taasisi na hata viongozi wa dini.
Kundi hilo lenye mtandao mpana nchini, linaonekana katika siku za karibuni kujikita katika mkoa wa Kilimanjaro.
Uchunguzi huo unaonyesha kuwa katika kipindi cha wiki mbili, watu wanne wamejikuta wakinaswa katika mtego huo na kutoa kitita cha kati ya Sh3 milioni na Sh10 milioni, gharama hizo zikiwa nje ya zile za kukomboa picha.
Kundi hilo hufanya kazi kwa kuwatumia wasichana wadogo na wakubwa, ambao wanaajiriwa maalumu kwa kazi hiyo ambayo haitofautiani na ya uchangudoa.
Mbali na waume za watu, wengine ambao wamenaswa kwenye mtego huo ni  baadhi ya mapadri wa Kanisa Katoliki, ambao hulazimika ‘kumalizana’ nao wakihofia kuchafuliwa kwa kashfa iwapo jambo hilo litaanikwa kwa umma.
Katika tukio la hivi karibuni, mfanyabiashara mmoja wa mjini Moshi alinaswa katika fumanizi hilo na mwanamke mmoja aliyedaiwa ni mkazi wa eneo la KDC Barabara Kuu ya Moshi-Himo na kulipa Sh3 milioni.
“Kwa hofu ya taarifa kumfikia mkewe, jamaa yangu aliamua kutoa fedha walizotaka, na unajua unapofumaniwa akili zinapotea kwa muda na unakuwa huna ujanja,” kilidokeza chanzo chetu.
Hata hivyo, chanzo hicho kilidai kuwa baada ya kupita wiki moja, mfanyabiashara huyo alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mwandishi wa gazeti moja la udaku akimtaarifu kuwa ana picha za mfanyabiashara huyo alizopigwa kwenye fumanizi.                                                                                                                                                                                                                                                                                                          
“Baada ya hapo tuliifuatilia namba yake na tumegundua anaitwa (jina tunalo), lakini kule kwenye lile gazeti hawamfahamu kabisa wala hiyo namba hawaijui,” alidai ndugu wa mfanyabiashara huyo.
Alidai kuwa, baada ya kumfuatilia mwanamke anayedaiwa kufumaniwa na ndugu yao, waligundua pia kwamba, tukio hilo ulikuwa ni mchezo mchafu.

No comments:

Post a Comment