ALIYEKUWA Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa yupo nchini Ujerumani kwa matibabu na uchunguzi wa kiafya.Lowassa
 ambaye pia ni Mbunge wa Monduli jana hakuwapo katika uzinduzi wa mradi 
wa Barabara ya Minjingu hadi Arusha na shule jimboni kwake, uliofanywa 
na Rais Jakaya Kikwete aliye ziarani mkoani Arusha.Kwa mujibu wa
 taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Jowika 
Kasunga na baadaye kusambazwa kwa waandishi wa habari, Lowassa alieleza 
kusikitishwa kutokuwapo jimboni kwake wakati huo ambao Rais Kikwete 
anatembelea jimbo lake.
Lowassa alisema kuwa, hali hiyo imetokana
 na kuwa safarini kwa ajili matibabu lakini akasema anaamini mambo 
yataenda vizuri si kwa ziara hiyo ya Rais Kikwete bali hata vikao vya 
juu vya CCM vinavyotarajiwa kufanyika hivi karibuni.
taarifa hiyo, alimsifu  Rais Kikwete kuwa, kutokana na kutekeleza vizuri
 na kwa uadilifu Ilani za uchaguzi za CCM, wiki mbili zijazo wanaCCM 
watakwenda Dodoma kuidhihirishia dunia  na Watanzania wenye shaka kwamba
 wanamwamini na kuuthamini uongozi wake.Katika maelezo hayo, Lowassa alieleza tatizo linalomsumbua kuwa ni macho, lakini pia atatumia nafasi hiyo kuchunguza afya yake.
Aidha,
 alimshukuru Rais Kikwete kwa kuzindua miradi hiyo akisema inadhihirisha
 mambo mawili makubwa aliyoyafanya kwa kiwango cha juu chini ya uongozi 
wake akiwa Rais wa Tanzania.“Mosi, chini ya uongozi wako shule 
nyingi zaidi zimejengwa kuliko awamu zote zilizotangulia. Pili, kilomita
 za barabara za lami zilizoongezeka wakati wa awamu yako ni ndefu kuliko
 wakati mwingine wowote,” alisema Lowassa na kuongeza:
“Kwa 
hakika umetekeleza vizuri, kikamilifu na kwa uadilifu Ilani za uchaguzi 
za CCM, mwaka 2005 na 2010. Sisi wanachama wa CCM na wananchi wa Monduli
 ni mashahidi wa jambo hili. Tunaamini ndivyo ilivyo kwa nchi nzima.”
Mwishoni
 mwa wiki ijayo CCM itafanya uchaguzi mkuu wa uchaguzi ngazi ya taifa 
kuanzia mwenyekiti wa chama na viongozi wengine, ili kukamilisha kupanga
 safu mpya ya uongozi kwa ajili  ya uchaguzi mkuu wa 2015.CCM 
ipo katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho ambapo tayari jumuiya zake 
za Wazazi, Vijana na Wanawake zimekamilisha chaguzi hizo, huku kambi ya 
Lowassa ikitajwa kuibuka kidedea kwa kunyakua nafasi mbalimbali 
zilizowaniwa, kuanzia ngazi za wilaya hadi jumuiya za chama kitaifa.
Katika
 uchaguzi wa UWT, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Taifa, Sophia Simba ambaye 
alitetea nafasi yake na Makamu wake, Asha Bakari Makame wanatajwa kuwa 
wafuasi wa Lowassa, huku wajumbe sita kati ya wanane  waliochaguliwa 
kuwakilisha jumuiya hiyo katika Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama 
hicho, wakiwa waumini wa kambi hiyo.
Wajumbe sita kati ya wanane
 walioshinda nafasi za ujumbe wa NEC kupitia jumuiya hiyo  wanatajwa 
kuwa wafuasi wa Lowassa,  huku mmoja akitajwa kuwa hana kundi lolote 
huku mwingine akitajwa kumuunga mkono aliyekuwa mgombea wa uenyekiti wa 
UWT na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Killango Malecela.Kwa 
upande wa UVCCM, Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamisi ambaye 
alichaguliwa kuwa Mwenyekiti kwa kura 483 na makamu wake, Mboni Muhita 
pia wanatajwa kuwa wafuasi wa kambi ya Lowassa.Waliotwaa ujumbe wa NEC na ujumbe wa Baraza Kuu la Umoja huo, pia wanatajwa kuwa waumini wa kambi hiyo.Hata
 hivyo, katika uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi uliokuwa wa funga dimba la 
mfululizo wa chaguzi za chama hicho tawala kuanzia ngazi za shina tangu 
Aprili, waliokuwa wagombea wa nafasi ya uenyekiti, John Barongo na 
Abdallah Bulembo kwa nyakati tofauti walikanusha kuwa na masilahi na 
makundi huku Martha Mlata akikataa kuzungumzia uchaguzi huo.
chanzo mwananchi jumapili 

No comments:
Post a Comment