Saturday, November 3, 2012

Binti:Baba mkwe alinikata masikio nilipokataa kuolewa

 
SERA ya  mtoto ya mwaka 1996 inasema kuwa mtoto ana haki ya kulindwa na kuendelezwa kielimu ili akue vyema kiakili, kimwili, koroho na kimaadili ili awe raia mwema anayewajibika kwake mwenyewe na taifa kwa jumla.
Hata hivyo hali hiyo ni tofauti kwa baadhi ya wazazi na walezi walio na jukumu la kutimiza hayo ambao huwageuza watoto kuwa ni miradi kwa kuwafanyisha kazi ngumu na biashara ndogo ndogo huku wengine wakikatisha masomo ya watoto hao na kuwaozesha.

Sikitiko Mateso(16), mkazi wa Mtaa wa Rosuti, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara ni mmoja wa watoto waliotendewa kinyume na sera hiyo ya mtoto, ambapo baba yake mzazi alimlazimisha kuolewa.
Akiwa ndiyo kwanza amehitimu elimu ya msingi mwaka huu wa 2012 katika Shule ya Msingi Mseto, wilayani Geita, mkoani Geita, Sikitiko alisoma kwa msaada wa Shirika la New Light Children Centre Organisation (NELICO), ndoto yake ikiwa kuwa Mwanasheria.

 Akizungumza na mwandishi wa makala haya mjini Geita, Sikitiko alisema kuwa yeye ni mtoto wa kwanza kati ya watoto tisa wa familia ya mzee Tamaa Mateso mkazi wa mjini Tarime, familia ambayo hutegemea vibarua vya kulima ili kupata mahitaji ya chakula, mavazi na mahitaji mbalimbali ya kifamilia na kwamba lengo kubwa la kuwa mwanasheria ni kujikita katika kupinga ukatili unaowakumba watoto.

Ndoto hiyo ya Sikitiko inatokana na kunusurika kifo, baada ya kufanyiwa ukatili wa kukatwa masikio na baba mkwe wake, baada ya kukataa kuolewa kwa nguvu na kijana wake wakati huo akisoma darasa la tatu Shule ya Msingi Roseti, wilayani Tarime mkoani Mara.

 Anasema kuwa baba yake, mzee Tamaa, aliandaa mazingira ya yeye kuolewa baada ya rafiki yake kumpa taarifa kwamba alikuwa anatafuta binti wa kuolewa na kijana wake, mazungumzo aliyodai yalifanyika kwenye klabu ya pombe za kienyeji.

 Akisimulia mkasa huo Sikitiko alisema kuwa akiwa na umri wa miaka 13 ambapo alikuwa darasa la tatu katika shule hiyo ya msingi, baba yake alikuwa akinywa pombe za kienyeji klabuni na rafiki yake aliyemtaja kwa jina moja la Kipanga.
 ‘’Huyo rafiki yake na baba, akamwabia baba yangu kwamba, ana kijana wake anataka kuoa. Baba akamwambia(rafiki yake), kwamba ampatie mahari kwani nyumbani kwake ana binti na ndiyo mimi. Hilo walikubaliana huko klabuni,’’alisema Sikitiko.
Baada ya makubaliano ya wazee hao, Tamaa aliporudi nyumbani alimwambia Sikitiko anayetambulika pia kwa jina la Rozi kwamba aolewe.

 ‘’Alipofika nyumani aliniita; “Rozi’’, akaniambia; “Mwanangu nataka uolewe.”
Anaongeza kuwa: “Nilikataa ombi la baba, nikamwambia mimi bado mdogo sana, pia ninasoma darasa la tatu hivyo, siwezi kuacha shule na kuolewa. Baba alikasirika sana.’’

Anaeleza kuwa baada ya kukataa ombi la kuolewa, baba yake alimpa amri akitaka aolewe kwa nguvu, huku akimwambia kwamba, atake asitake, ataolewa na huyo kijana mkazi wa Nyamihutwa Tarime, aitwaye Luis Kipanga .
Sikitiko alisema kuwa baba yake alivyozidi kuwa mkali baada ya yeye kukataa ombi lake, Juni 2008 aliamua kutoroka nyumbani kwao na kuanza safari ya kutembea kwa miguu muda wa saa 11  kwenda kwa mjomba wake eneo la Chibumbai, Tarime.

Hata hivyo, anasimulia kuwa wakati akitoroka, baba yake alikuwa tayari ameshapokea mahari ya Sh300,000 kutoka kwa rafiki yake ili yeye (Sikitiko) aache shule na kwenda kuolewa na kijana huyo.
Anabainisha kuwa baada ya mzee Tamaa kupokea mahari hiyo, mzee Kipanga alimbana ili amtoe yeye kwa ajili ya ndoa,  kwani kijana wake(Luis), alikuwa ameshajiandaa kwa mapokezi na kuoa.
 Hata hivyo, jitihada za Sikitiko kujiokoa na janga hilo kwa kutoroka nyumbani kwao na kwenda kuishi mafichoni kwa mjomba wake, hazikuzaa matunda kutokana na baba yake kumsaka kila wanapoishi ndugu zake hadi alipomkuta kwa mjomba wake.

No comments:

Post a Comment