Saturday, November 3, 2012

TIC yatoa somo kwa wajasiriamali kufanikisha biashara

MWENYEKITI  wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Balozi Elly Mtango ametoa somo kwa wafanyabiashara wajasirimali nchini na kuwaeleza kuwa siri ya mafanikio katika biashara yoyote ni uwezo, juhudi na mtazamo.
Alisema hayo alipozungumza katika sherehe fupi za kutoa vyeti kwa wajasiriamali walioshinda mpango wa kuandaa miradi inayohusiana na biashara za nishati zilizoandaliwa na taasisi inayotoa huduma za maendeleo ya ujasiriamali na biashara ya SEED.
Balozi Mtango alisema kanuni za mafanikio yoyote ni juhudi za mhusika na akawataka wajasiriamali kutumia mbinu tofauti zitakazoziwezesha biasharaa zao kufanikiwa na kuifanya miradi yao iwe endelevu.
“Zaidi ya uwezo na jitihada ni muhimu pia kuwa na mtazamo, kadiri mtu anavyozidisha mtazamo chanya na ari ya kutenda jambo, ndivyo hivyo maisha yake yanavyokuwa na ufanisi zaidi,” alisema Balozi Mtango.
Alisema watu wengi wanazo ndoto za kufanya mambo makubwa katika maisha yao, lakini akasema ndoto zinaweza kutimia kwa kufanya kazi kwa bidiii na sio kwa njia ya mkato.
“Bila jitihada, ndoto nzuri sana itabaki bila kukamilishwa, katika safari ya maisha hakuna muujiza, tunapaswa kutembea hatua moja kwa wakati, tunapaswa kuwa na subira, jitihada za kila siku huleta ushindi,katika maisha na kwenye biashara yoyote, hatua moja kwa wakati ndio njia pekee ya uhakika ya kubadili ndoto kuwa jambo la kweli” alisema
Akizungumza katika sherehe hizo,  Mkurugenzi Mtendaji wa SEED, Msafiri Chagama alisema taasisi yake imekuwa katika mpango wa kuwajengea uwezo wafanyabiashara wajasiriali na kuchagua wale wanaoshughulika na biashara za nishati.
Alisema jumla ya kampuni 73 za wajasiriamali zilijitokeza kushiriki katika shjindano hilo  ambapo baada ya mchuzo zilipatikana 53 zilizoshindanishwa kabla ya kupata washindi 15  kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Alisema kati ya 15 waliopatikana, washindi wanne walipata zawadi ya kutembelea nchini Uholanzi ambapo watapata fursa ya kujifunza zaidi kuhusu shughuli mbalimbali zinazoohusu biashara pamoja na kupata uzoefu kutoka kwa wenzao wanaofanya biashara kama zao nchini humo.
Aliwataja washindi hao ambao watakaa Uholanzi kwa wiki nzima kuwa ni Godfrey Mosha, Lawrence Makenya, Cuthbert Kajuna na Mshindwa Edith Banzi.
Alisema washindi hao vile vile watapata fursa ya kushiriki katika maonyesho na kuonyesha kile wanachokifanya katika biashara za nishati.
Alisema wale washiriki wengine ambao hawakupata fursa ya kwenda uholanzi watasaidiwa ushauri na jinsi ya kuboresha biashara zao.

No comments:

Post a Comment