MWENENDO wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne
Makinda, kukalia taarifa za utekelezaji wa maazimio mbalimbali ya
Bunge, unamweka katika wakati mgumu, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Hadi sasa taarifa za utekelezaji wa maazimio makubwa matano
zimekaliwa, kubwa ikiwemo ripoti inayohusu utekelezaji wa maagizo ya
Bunge kuhusu tuhuma zinazomkabili aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, David Jairo na taarifa ya Kamati ndogo ya Bunge ya
uchunguzi dhidi ya wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini, iliyoongozwa
na Mbunge wa Mlalo, Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi (CCM).
Kamati ya Ngwilizi tayari imeshakabidhi taarifa yake kwa Spika Makinda, lakini hadi sasa inafanywa kuwa siri.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa, taarifa ya ripoti
ya Ngwilizi haitaletwa bungeni licha ya presha kutoka kwa wabunge, hasa
wa Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa.
Sababu inayotajwa ya kutowasilisha taarifa hiyo bungeni, ni kutokana na madai kuwa ripoti hiyo imechakachuliwa na mafisadi.
Wiki iliyopita, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) alitoa hoja ya
jambo linalohusiana na Haki za Bunge kwa mujibu wa kanuni ya 55 (3) (f)
na 59 (e) ya kutaka Bunge lipewe haki yake kwa haraka ya kupewa taarifa
na Spika juu ya hatma ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa
kuzingatia kuwa tayari amekabidhiwa ripoti ya Kamati ya Ngwilizi.
Mnyika alieleza kwamba, matatizo ya mafuta na gesi asili yanayoendelea
sasa ni matokeo ya udhaifu wa serikali katika kutekeleza maazimio na
mapendekezo ya Bunge, huku kukiwa hakuna Kamati ya Bunge ya Nishati na
Madini ili kuweza kuisimamia serikali kwenye sekta ya nishati, na hivyo
kuathiri uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.
Iwapo hoja hiyo iliyoungwa mkono ingejadiliwa, Spika angelazimika
kueleza hatma ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, na kwa kufanya
hivyo angelazimika pia kueleza ni kwanini ripoti ya kamati juu ya tuhuma
za wabunge haijawasilishwa bungeni na ni lini itawasilishwa.
Mbali ya taarifa ya Kamati ya Ngwilizi, uchunguzi umebaini kuwa,
katika kipindi cha kati ya mwaka 2008 hadi sasa, Bunge limeshindwa
kupata taarifa ya maazimio makubwa matano ambayo hayajatekelezwa kwa
ukamilifu, na Spika hajasimamia kuhakikisha Bunge ama kwa kupitia kamati
zake, linapatiwa taarifa.
Taarifa ya serikali inayosubiriwa kwa hamu bungeni ni ile inayohusu utekelezaji wa maagizo ya Bunge kuhusu tuhuma za Jairo.
Ikumbukwe kwamba, Novemba 2011, Bunge lilipitisha maazimio ya hatua za
kuchukuliwa baada ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza
uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha
kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011.
Kumbukumbu za Bunge zinaonyesha kuwa, Spika Makinda aliikataa taarifa
ya ripoti hiyo kwa vile majibu ya serikali hayakumridhisha.
Hata hivyo, hadi sasa hajaitaka serikali kuwasilisha taarifa hiyo
kwenye mikutano iliyofuata kuanzia ule wa bajeti wa mwezi Juni mpaka
Agosti 2012 na hata huu wa sasa unaoendelea, ratiba inaoonyesha kwamba
taarifa ya Jairo imewekwa kabatini.
Tuhuma dhidi ya Jairo ziliibuka wakati Wizara ya Nishati na Madini
ilipokuwa inawasilisha bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/12 ambapo Mbunge
wa Kilindi, Beatrice Shelukindo (CCM) alidai kuwa alichangisha sh
bilioni moja kutoka kwenye taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara
yake kwa ajili ya kusaidia kupitisha bajeti hiyo.
Baada ya madai hayo, serikali ilichunguza suala hilo kupitia Ofisi ya
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utoah, na
hatimaye uamuzi kutangazwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon
Luhanjo, kuwa Jairo hakuwa na makosa na akamwamuru arejee kazini.
Bunge halikuridhika na hali hiyo na kuunda Kamati Teule ya Bunge
ambayo ilimtia Jairo hatiani na kupendekeza maazimio mbalimbali ya
serikali kutekelezwa ambayo mpaka sasa serikali haijaeleza bungeni
utekelezaji wake.
Akizungumzia suala hilo jana, Mnyika ambaye pia ni Waziri Kivuli wa
Nishati na Madini, alisema kuwa inaonyesha kwamba serikali bado haioni
uharaka na ulazima wa kuchukua hatua, hivyo ni muhimu Spika atumie
madaraka na mamlaka yake kuiagiza iwasilishe ripoti hiyo bungeni.
“Wakati Bunge lilipokaa kama kamati tarehe 28 Julai 2012 kupitisha
bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, nilitaka ufafanuzi kutoka kwa
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kuhusu
utekelezaji wa maazimio hayo ambayo mpaka sasa hakuna taarifa ya
utekelezaji iliyowasilishwa bungeni tangu yapitishwe Novemba mwaka 2011.
“Waziri akajibu tu kwamba hawezi kufanyia kazi taarifa za magazetini,
bila kujali kwamba nilichouliza hakihusu taarifa za magazetini bali
maazimio ya Bunge baada ya kazi iliyofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali, na ikarudiwa tena na Kamati Teule ya Bunge ambayo ilihoji
wahusika na kupata pia vielelezo. Spika anapaswa kuchukua hatua,”
amefafanua Mnyika.
chanzo-Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment