Thursday, November 8, 2012

TFF: Hatuibebi Yanga

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limetoa ufafanuzi juu ya madai ya klabu ya Simba kuwa inaibeba Yanga katika Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na mabadiliko ya ratiba iliyoifanya hivi karibuni.
Katika mabadiliko hayo, mechi zote za kufunga mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zilizokuwa zifanyike Jumapili, zilihamishiwa Jumamosi (kesho), huku ile ya Yanga ikibaki Jumapili kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, jambo lililolalamikiwa na uongozi wa Simba, kwa madai ni upendeleo kwa watani wao.
Simba waliandika barua TFF, wakitaka wacheze siku moja na Yanga na kudai, kwa nini mechi zote zirejeshwe nyuma ya Yanga pekee ibaki siku hiyo.
Akilitolea ufafanuzi suala hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Ligi, Wallace Karia, alisema sababu za mchezo wa Yanga kubaki Jumapili ni kutokana na Uwanja huo wa Mkwakwani, Jumamosi kutumika kwa mchezo mwingine wa ligi hiyo, kati ya wenyeji Mgambo JKT na Azam FC ya Dar es Salaam.
“Sisi tuliangalia sana hii ratiba, maana Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen, aliomba ratiba ibadilishwe kutokana na timu ya taifa kuingia kambini Jumapili na sisi tukaamua kufanya hivyo na hata kama tungesema Azam wacheze kesho Jumamosi, tusingewatendea haki kwa kuwa jana tu walikuwa na mechi,” alisema Karia.
Aidha, Karia alisema hata hiyo barua ambayo Simba wanadai wameiwasilisha TFF, yeye hajaiona na hatokuwa na muda wa kuipitia kutokana na sababu za kubadilisha ratiba hiyo kuwa wazi.
Aliongeza malalamiko ya Simba hayana msingi kwa kuwa hawaweki maslahi ya taifa mbele na kudai kuwa waliona ni vema kubadilisha mechi hizo ambazo ni nyingi na zingeweza kuleta usumbufu kutokana na wachezaji walioteuliwa kuchelewa kuungana na wenzao Stars.
Naye Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema Simba wanatakiwa kuwa na utaifa kwanza kwa kuwa madai yao hayana maana na haina jinsi siku moja katika uwanja mmoja zikachezwa mechi mbili.
Ligi Kuu raundi ya mwisho ilitakiwa kufikia tamati Jumapili, na kurejeshwa nyuma siku moja na mechi zitapigwa katika viwanja sita tofauti ambapo Azam watacheza na Mgambo JKT katika Uwanja wa Mkwakwani Tanga, African Lyon na Mtibwa Chamazi.
Mechi nyingine Simba na TotoAfrican Taifa, Tanzania Prison na JKT Ruvu Sokoine Mbeya, Kagera Sugar na Polisi Morogoro Kaitaba, JKT Oljoro na Ruvu Shooting Amri Abeid na Yanga na Costal Union wakicheza Jumapili Mkwakwani Tanga.

No comments:

Post a Comment