Thursday, November 8, 2012

MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), amemlipua hadharani Waziri Mkuu,fuatilia mvutano huo ulioamuliwa na Mbowe

MBUNGE wa Kawe, Halima Mdee (CHADEMA), amemlipua hadharani Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akidai ni miongoni mwa viongozi wa ngazi za juu ambao wametajwa kuhusika katika kushinikiza ugawaji huo wa ardhi.
Mdee ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alitoa kauli hiyo bungeni jana wakati akiwasilisha hoja binafsi inayolenga kuitaka Serikali kusitisha ugawaji wa ardhi kwa wawekezaji kutokana na hofu wanayoipata katika mazingira yasiyo halali ikiwamo kuwatumia vigogo serikalini.
Alisema katika baadhi ya maeneo nchini, uwekezaji umekuwa ukifanywa kutokana na shinikizo la viongozi wa ngazi za juu serikalini huku pia akiwataja wawekezaji waliogeuka kuwa ni matatizo.
Katika hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wa upinzani na pomoja na wawili wa CCM, Lekule Laizer (Longido) na Dk. Faustine Ndugulile (Kigamboni), Mdee alitaka ugawaji ardhi kwa wawekezaji wa nje na ndani usitishwe hadi hapo tathimini ya kina itakapofanyika kubaini ni kiasi gani kipo mikononi mwa wawekezaji.
Hoja hiyo pia inataka tathmini ya kina ifanyike kuweza kubaini raia wa kigeni na wa ndani waliojipatia ardhi kinyemela kupitia Serikali za vijiji kinyume na matakwa ya sheria ya ardhi Na. 5 ya mwaka 1999.
Mdee alisema kwa muda mrefu kumekuwapo na uwekezaji usiokuwa na tija kwa taifa, hivyo akawataka wabunge kuunga mkono hoja yake ili kunusuru taifa.
Alisema kumekuwa na ubabaishaji mkubwa katika sekta hiyo na kwamba katika mazingira mengine Serikali imekuwa kuwadi wa wawekezaji.
Mdee alisema inakadiriwa kuwa kati ya mwaka 2001 hadi 2010 kulikuwa na maombi ya wawekezaji kutaka ardhi zaidi ya hekta milioni 203 katika nchi zinazoendelea barani Afrika.
“Hii ni sawa na maombi ya hekta 55,616 kila siku katika kipindi cha miaka 10. Halikadhalika nchini Tanzania katika miaka ya karibuni takriban hekta milioni nne zimeripotiwa ‘kuombwa’ na wawekezaji wa nje kwa kilimo cha mazao ya mafuta na chakula.
“Mheshimiwa Spika, ninaliomba Bunge lako tukufu, likubaliane na hoja ya kuitaka Serikali kusitisha ugawaji wa ardhi ili kuweza kutoa fursa kama nchi kuweza kujitahmini kwa kina, wapi tulikosea ili tuweze kujipanga upya kwa manufaa ya nchi na wananchi,” alisema.
Hata hivyo, Mdee alisema hakuna anayepinga umuhimu wa uwekezaji, lakini ni muhimu vile vile ikaeleweka kuwa taifa haliwezi kuendelea kukabidhi kila kitu kwa wageni.
“Sote tunajua ni kwa namna gani dhahabu, almasi na Tanzanite zimetumika kujenga uchumi wa mabeberu! Hatuwezi kufanya makosa tena kwenye rasilimali hii muhimu ya ardhi inayopanda thamani kwa kasi sana. Uchumi hauwezi kuachwa uendeshwe na watu wa nje,” alisema.
Kwamba kuna haja kubwa kwa wabunge kutambua kuwa matatizo ya ardhi yanayoikumba Rufiji, Kilombero, Bagamoyo, Kisarawe na Lugufu yanaikumba pia Muheza, Pangani, Katavi, Meatu, Kinondoni, Njombe na Ngorogoro.
“Maeneo mengi ardhi yanayochukuliwa na wawekezaji hao huwa hayaendelezwi kama inavyopasa na yale ambayo yanaendelezwa, yanaendelezwa kwa kiwango kidogo sana huku wananchi wengi wakiachwa pasi na ardhi ya kutosha kwa kilimo.
“Katika hatua nyingine, wawekezaji baada ya kupata /kumilikishwa ardhi kwa bei ya kutupa, hawaitumii, wanasubiri ipande thamani, kisha kuiuza kwa faida kwa wawekezaji wengine,” alisema.
Mdee alisema Kampuni ya kimarekani ya Agrisol imepewa eneo kubwa mkoani Rukwa linalohusisha hekta 80,317 (Katumba) na 219,800 ( Mishamo).
”Katika eneo hili majadiliano yanaratibiwa na viongozi wakubwa sana serikalini. Mradi huu umejikita kwenye uendelezaji wa mashamba makubwa na matumizi ya mbegu zenye viini tete (GMO).
Kwa upande wa Mkoa wa Kigoma, alisema maeneo makubwa ya ardhi yameuzwa kwa kampuni za AGRISOL na FELISA.
Alisema FELISA amenunua ekari 3,000 katika Wilaya ya Uvinza Kijiji cha Basanza Kata ya Uvinza. Wawekezaji hawa wamewakuta wakulima na wafugaji katika maeneo haya.
“Mwekezaji wa AGRISOL amepewa hekta elfu 10,000 eneo la Lugufu. Eneo hili ndio ili kuwa kambi ya wakimbizi. Eneo hili ndio limetengwa kuwa makao makuu ya wilaya,” alisema.
Mdee alifafanua kuwa kwa kuwa rasilimali ardhi ndio urithi pekee wa asili ya Mtanzania katika kujitafutia riziki na kuendesha maisha yake uwekezaji katika ardhi unaofanywa na makampuni ya nje haujawasaidia wananchi kwa maana ya fursa za ajira na upatikanaji wa chakula, analiomba Bunge liazimie kusitiza ugawaji huo.
Baadhi ya wabunge waliochangia waliunga mkono hoja hiyo, huku wakisema kuwa migogoro ya ardhi ni tatizo sugu nchini na kwamba limetokana na kiwango kidogo cha ardhi kilichopimwa.
Laizer katika mchango wake alisema suala la ardhi halina itikadi ya kichama, hivyo akawataka wabunge wenzake kuunga mkono hoja hiyo ili kutoa fursa kwa taifa kujipanga na kufanya tahimini upya.
Naye Waziri wa Mahusiano, Steven Wassira, alisema kuwa anakubaliana na hoja ya Mdee ya kufanya upya tathimini huku akisisitiza kuwa wakiendelea na mfumo uliopo ambao umejaa rushwa, watabaki bila ardhi.
“Huko kwenye ngazi ya vijiji, kuna watu wanapigwa rushwa kijiji kilichokaa kupitisha ardhi kina majina ya marehemu na sahihi zao mimi nafanya kazi Ikulu haya mambo yapo,” alisema Wassira.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk. Mary Nagu, naye alisema kuwa hawawezi kukataa wawekezaji ambao wanafuata taratibu huku akisisitiza kuwa wapo wasio matapeli.
Hata hivyo, kabla ya hoja ya Mdee haijafanyiwa mabadiliko na kupita, Waziri wa Ardhi, Prof. Anna Tibaijuka, aliomba azimio hilo libadilishwe badala ya kusitisha ugawaji ardhi ibaki hoja ya kufanya tathimini tu ambayo itabaini wawekezaji wa raia wa kigeni waliojipatia ardhi kinyemela. Kauli hiyo ilizua mjadala kwa wabunge wa upinzani wakikataa huku wale wa CCM wakiunga mkono.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) aliungana na Mdee akisema kuwa hoja ya kusitisha haihitaji fedha ila tathimini ndiyo inayohitaji fedha.
“Ukiruhusu tathimini wakati bado unaendelea kugawa ardhi, utakuta umegawa yote. Halima alikuwa muungwana hakusema wawekezaji wanyang’anywe,” alisema. Msimamo huo wa Zitto ulionekana kuungwa mkono na wabunge wengi wa upinzani huku mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka aliyekuwa akiungwa mkono na wenzake wa CCM alipinga hali ambayo iliendelea kuzua mjadala.
Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu wa Bunge) William Lukuvi, alilazimika kusimama akisema serikali inaunga mkono hoja hiyo na kwamba kama wangekuwa hawaiungi mkono wangekataa kwani kanuni inawaruhusu.
Lukuvi aliwataka wabunge waunge mkono hoja ya kufanya tathimini tu na kuasa kuwa endapo watasimamisha ugawaji ardhi kuna watu watakwenda mahakamani na kuhoji kwanini wanataka kujifedhehedha.

No comments:

Post a Comment