Thursday, November 8, 2012

CT Scan ya Muhimbili mbovu JIBU LA SWALI LA MBUNGE Viti Maalum

SERIKALI imekiri kipimo cha CT-SCAN kilichokuwa kikitumika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kimeharibika, hivyo kuleta usumbufu mkubwa kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Husein Mwinyi, alitoa kauli hiyo bungeni alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalumu, Getrude Rwakatare (CCM).
Katika swali hilo, mbunge huyo alihoji mpango wa serikali katika kununua kifaa kipya cha CT-SCAN, ili kuwasaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo hapa nchini.
“Serikali ipo tayari kuwaongezea sh 70,000, ili kuwasaidia wagonjwa ambao wanahitaji huduma hiyo kwenda kutibiwa katika hospitali binafsi ya Regency na Agakhan?” alihoji.
Akiendelea kujibu swali hilo, Dk. Mwinyi alisema awali walitengeneza kipimo hicho ambacho hivi sasa kimeharibika tena.
“Wizara yangu imeanza kuchukua hatua na imeiagiza bima ya afya kutoa fedha kwa ajili ya kununua kipimo kipya, ili kuwaondolea adha wagonjwa,” alisema Dk. Mwinyi.
Aidha alisema kwa sasa serikali haina fedha ya kuwaongezea wagonjwa hao ambao wanahitaji huduma ya CT-SCAN, ili wakatibiwe katika hospitali hizo binafsi bali inaharakisha mchakato wa kuagiza kipimo hicho ili huduma hiyo iweze kurejea kama kawaida.
Katika swali la msingi, mbunge huyo alihoji ni kwa nini serikali isiboreshe maslahi ya madaktari hao, ili kuwavutia wabakie hapa nchini kutoa huduma kwenye hospitali mbalimbali.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alisema kwa kutambua tatizo, serikali imeboresha mishahara kwa kutoa nyongeza ya zaidi ya asilimia 400 ya kiwango walichokuwa wakilipwa awali.
Alifafanua kuwa mshahara wa daktari kwa mwaka 2005-2006 ulikuwa sh 267,480 kwa mwezi ambapo katika kipindi cha mwaka 2012-2013 umekuwa sh 1,102,000 kwa mwezi sawa na ongezeko la asilimia 412.

No comments:

Post a Comment