Wednesday, November 7, 2012

Ponda abaki rumande • Wenzake wapata dhamana, wengine 11 washtakiwa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, jana iliwapatia dhamana washtakiwa 49 wanaokabiliwa na kesi ya uchochezi na wizi wa mali za sh milioni 59, huku Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda Issa, akiendelea kusota rumande.
Hatua ya Ponda kuendelea kusota rumande inatokana na uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Dk. Eliezer Feleshi, kuwasilisha mahakamani hapo hati ya kufunga dhamana ya mshtakiwa huyo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kwa ajili ya usalama na maslahi ya taifa.
Hata hivyo, wakati watuhumiwa hao 49 wakipatiwa dhamana, watu wengine 11 waumini wa dini ya Kiislamu wamefikishwa mahakamani hapo, wakikabiliwa na makosa mawili ya kukaidi amri ya Jeshi la Polisi, iliyowataka wasifanye mkutano na kuvuruga amani.
Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Victoria Nongwa, ndiye alitoa dhamana kwa mshtakiwa wa 2-50 wa kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi zenye thamani ya sh milioni 56 mali ya Kampuni ya Agritanza Ltd inayomkabili Sheikh Ponda na wenzake.
Alisema masharti ya dhamana yalikuwa ni ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima awe na mdhamini mmoja wa kuaminika atakayesaini bondi ya sh milioni moja.
“Nimelidhika washtakiwa wote mmetimiza masharti ya dhamana, hivyo nawapatia dhamana, mtakuwa nje kwa dhamana na dhamana hiyo haitamhusu mshitakiwa wa kwanza, Sheikh Ponda ambaye dhamana yake imefungwa na DPP,” alisema Hakimu Nonga na kuahirisha kesi hiyo hadi Novemba 15, mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya upande wa jamhuri kuwasomea washitakiwa hao maelezo ya awali.
Kuhusu washtakiwa wapya, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Shadrack Kimaro mbele ya Hakimu Mkazi, Liad Chamshama, aliwataja kuwa ni Salum Shabani, Salum Mkulega, Ernest Silvester, Josephat Alocye, Edwin Sadoki, Stanley Nhonya, Athumani Sajuki, Thabit Kombo, Abdully Rashid na Niga Ndiganga.
Alidai shitaka la kwanza ni la kudharau amri halali ya polisi, kwamba Novemba 2 mwaka huu, huko Mtaa wa Tandamti katika Msikiti wa Idrisa jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walikaidi amri hiyo waliyopewa ikiwakataza wasifanye mkusanyiko wowote.
Chamshama alilitaja shtaka la pili kuwa ni la kufanya mkusanyiko haramu kinyume na sheria ambapo Novemba 2 mwaka huu, eneo la mtaa wa Tandamti katika Msikiti wa Idrisa, washitakiwa hao kwa pamoja wakiwa na nia ovu walifanya mkusanyiko haramu ambao ulisababisha kuvuruga amani katika eneo hilo na upelelezi bado haujakamilika.
Hata hivyo, washitakiwa hao walikana mashitaka hayo na kupelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana kila mmoja kuwa na wadhamini wawili toka ofisi zinazotambuliwa na serikali, ambao kila mmoja atasaini bondi ya sh milioni tano.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Novemba 20, mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

No comments:

Post a Comment