Wednesday, November 7, 2012

Azam FC waishusha Simba baada ya kuifunga Oljoro JKT

AZAM FC ‘Wana lambalamba’ jana walizidi kuongeza machungu Msimbazi, baada ya kuibuka na ushinmdi wa bao 1-0 dhidi ya Oljoro JKT ya Arusha na kukwea hadi nafasi ya pili iliyokuwa ikikamatwa na Simba katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.
Kwa ushindi huo wa Azam uliopatikana kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Chamazi Complex, imefikisha pointi 24 ndani ya mechi 12 na kuishusha Simba yenye pointi 23 huku vinara Yanga wakiwa na pointi 26.
Azam ilijipatia bao dakika ya nne likifungwa na Kipre Tchetche kwa penalti, baada ya Yasin Juma kuunawa mpira katika eneo la hatari na mwamuzi Livingstone Lwiza kutoka Kagera kuamuru lipigwe tuta.
Licha ya kosa kosa za hapa na pale, hadi mapumziko Azam walikuwa mbele kwa bao hilo moja.
Kipindi cha pili, timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu, lakini dakika ya 88, Himid Mao wa Azam alilimwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Amir Omari. Hadi dakika 90 zinakamilika, Azam waliibuka wababe.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Wagosi wa Kaya, Coastal Union waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya vibonde Polisi Morogoro.
Bao la Wagosi lilifungwa na Daniel Lyanga dakika ya 15, akimalizia mpira uliopigwa na Kassim Selemani ‘Selembe’. Kwa ushindi huo, Coastal imefikisha pointi 22 na kukamata nafasi ya nne.
Azam FC: Mwadini Ali, Himid Mao, Lackson Kakolaki, Aggrey Morris, Waziri Salum, Salum Abubakari, Kipre Balou, Jabir Aziz, Hamis Mcha ‘Viali’, John Boko, Kipre Tchetche.
Oljoro JKT: Rucheke Musa, Yasin Juma, Omary David, Salim Mbonde, Marcus Raphael, Emmanuel Memba, Karage Gunda, Idd Swalehe, Amir Omari, Meshack Nyambele, Esau Mwaseba.

No comments:

Post a Comment