Wednesday, November 7, 2012

Hatma ubunge wa Lema leo

HATIMA ya rufaa ya kesi ya aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini kupitia Chadema, Godbless Lema, itajulikana leo wakati Mahakama ya Rufani, itakapotoa uamuzi kuhusu pingamizi lililowekwa na upande wa wajibu rufaa dhidi ya rufaa hiyo.

Lema alivuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha April 4 mwaka huu, kufuatia kesi iliyofunguliwa na wanachama watatu  wa CCM, wakipinga ushindi wake katika uchaguzi mkuu mwaka 2010.
Godbless Lema,


Wanachama hao ni  Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel.

Hata hivyo , kupitia kwa Wakili wake Method Kimomogoro, Lema  alikata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, huku akiorodhesha hoja 18 za kuipinga.

Siku ambayo rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa na jopo la  Majaji watatu Mahakama ya Rufani wakili wa wajibu rufaa, Alute Mughwai, aliweka pingamizi la awali.

Jopo linalosikiliza kesi hiyo linawajumuisha Jaji  Salum Massati, Jaji  Natalia Kimaro  na  Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande.

Katika pingamizi hilo, Wakili Mghwai aliiomba mahakama, iitupile mbali rufaa hiyo, akidai  kuwa ina kasoro za kisheria na za kikanuni, jambo ambalo  liliibua mvutano wa hoja za kisheria baina ya pande zote.

Habari zilizolifikia Mwananchi kutoka mahakamani na kuthibitishwa na Afisa Habari wa Mahakama, Mary Gwao, kwa niaba Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Zahra Maruma zilisema  uamuzi wa pingamizi hilo utatolewa leo asubuhi.

Awali uamuzi wa pingamizi hilo ulipangwa kutolewa Novemba 29 mwaka huu, lakini baadaye rufaa hiyo ikaondolewa katika orodha ya kesi ambazo zilipangwa kusikilizwa na kutolewa uamuzi katika vikao vya Mahakama ya Rufani vya  Novemba.

Maruma alisema kuwa uamuzi wa pingamizi hilo uliondolewa kwenye orodha ya kesi ambazo zilipangwa tarehe hiyo kwa kuwa ungeweza kukamilika wakati wowote hata kabla ya siku hiyo.
Habari zilizopatikana kutoka duru za Kimahakama na kuthibitishwa na Wakili wa Mrufani, Method Kimomogoro, zimeeleza kuwa uamuzi huo utatolewa Jijini Dar es Salaam baada ya jopo la majaji watatu waliosikiliza pingimizi hizo kukamilisha kupitia hoja za mawakili.
Pingamizi hizo zilisikilizwa Jijini Arusha wakati wa kikao cha Mahakama ya Rufaa kilichofanyika jijni Arusha mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu.
Akizungumza kwa njia ya simu, Wakili Method Kimomogoro anayemwakilisha Lema katika rufaa hiyo akishirikiana na Mwenzake Tindu Lissu alithibitisha kupokea hati ya kuitwa mahakamani kusikiliza uamuzi huo leo Alhamisi.“Ni kweli nimetoka kuchukua wito wa kufika mahakamani sasa hivi inayotuagiza kufika mbele ya Mahakama ya Rufaa Alhamisi kusikiliza uamuzi wa pingamizi za rufaa ya mteja wetu Novemba 8, mwaka huu,”
alisema Kimomogoro.

No comments:

Post a Comment