Wednesday, November 7, 2012

MWENYEKITI wa Bunge, Sylvester Mabumba, jana alionekana kutumia kiti cha Spika kuliyumbisha Bunge

MWENYEKITI wa Bunge, Sylvester Mabumba, jana alionekana kutumia kiti cha Spika kuliyumbisha Bunge kutokana na kile kilichoonekana kukosa msimamo wa kutoa maamuzi.
Hali hiyo ilitokea jana wakati Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbalawa na Naibu wake January Makamba, wakitaka kuwasilisha azimio la kutaka Bunge liridhie Mkataba Mpya wa Umoja wa Posta Afrika.
Kabla ya waziri huyo na naibu wake hawajawasilisha azimio la mkataba huo mpya, alisimama Mbunge wa Mwibara, Alphaxard Kangi Lugola, akitumia kanuni ya (68) 7 akimtaka Mwenyekiti Mabumba asiruhusu wabunge kujadili mkataba huo kwa muda huo, kwa sababu hakukuwa na mbunge hata mmoja aliyekuwa na mkataba.
Lugola badala yake alimtaka mwenyekiti huyo ambaye alikuwa akiongoza Bunge jana, aruhusu waziri asome mkataba huo kisha kuahirisha shughuli za Bunge hadi jioni ambapo wabunge watakuwa wamekwishausoma baada ya kuwa wameupata.
Baada ya maelezo ya Lugola, mwenyekiti huyo alikubali kupokea ombi hilo la muongozo na kusema kuwa, atawasiliana na wenzake akiahidi kutolea maamuzi muda mfupi.
Kauli hiyo ya Lugola iliwafanya wabunge wengi washangilie, lakini hata hivyo baada ya muda mfupi, Mabumba ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Gole (CCM), alimruhusu waziri asome azimio la mkataba huo mpya, wakati huo wabunge wakiwa wanagawiwa vitabu.
Baada ya waziri kumaliza kuusoma na kisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kumaliza kuwasilishwa, alisimama Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM) akimtaka mwenyekiti kuruhusu wabunge kuchangia kwa sababu kazi ya kuusoma na kuupitia mkataba huo ilikwishafanywa na kamati yake ambayo ilifanya kazi kwa ajili ya Bunge zima.
Baada ya Serukamba kuzungumza hayo, alisimama Mabumba na kulieleza Bunge kuwa, aliletewa karatasi ya maandishi na kamati na kumponda Lugola kwa kuongea vitu asivyovijua na kuwaomba wabunge waendelee kujadili.
“Meza ililetewa karatasi ya maandishi na kamati, mimi nasema wabunge tusipende kutoa hoja tusizozijua… wanasema kama kitu hujui ni bora unyamaze kuliko kupotosha Bunge, wabunge ninaomba tuendelee kujadili, naondoa ile hoja ya kuzuia wabunge wasijadili kwa sababu Kamati ya Bunge ilipitia mkataba huu kifungu kwa kifungu,” alisema Mabumba.
Baada ya kusema hayo, alisimama Waziri Kivuli wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Joshua Nassari na kuwasilisha maoni ya kambi ya upinzani.
Hata hivyo, kigeugeu hicho cha Mabumba kilionekana kumkera Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM) ambaye wakati akichangia kuhusu mkataba huo, alianza kwa kumshutumu Mabumba kwa kuliyumbisha Bunge.
“Nasikitika kiti kilivyoyumbishwa leo… Mwenyekiti naomba niseme tu kwamba unayumbisha Bunge, hatuwezi kwenda kwa utaratibu huu,” alisema Zambi ambaye pia aliendelea kuchangia azimio lililoko mezani.
Baada ya Zambi kumaliza kuchangia, Mabumba alisimama na kumwambia kuwa, kauli yake kwamba kukalia kwake kiti kunayumbisha Bunge si kweli, na kwamba hajamtendea haki.
Wakati Mabumba akizungumza hayo, ghafla mbunge mmoja ambaye hakujulikana, aliwasha kipaza sauti na kusema haina haja huku Mabumba naye akimjibu akimwambia; “naomba unyamaze”.
Awali, wakichangia azimio la mkataba huo ambao serikali inasema ina lengo la kuboresha huduma za posta nchini, wabunge waliitadharisha serikali kuwa makini na kuishauri kabla kukimbilia kujiunga kwenye mkataba huo, iangalie jinsi ya kuimarisha Shirika la Posta nchini kwani hali yake ni mbaya.
Aidha, baadhi ya wabunge walihoji mkataba huo kuletwa bungeni leo wakati taratibu za kuanza kuusaini zilianza takribani zaidi ya miaka 30 iliyopita, na kutilia shaka kama utakuwa unaendana na wakati wa sasa ambako teknolojia iko juu.
chanzo-Mtanzania daima

No comments:

Post a Comment