Friday, November 2, 2012

Mkurugenzi TANESCO afukuzwa • Akutwa na makosa ya ukiukwaji taratibu

HATIMAYE Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO), imemtimua kazi aliyekuwa Mkurugenzi wake, Mhandisi William Mhando, baada ya kumtia hatiani kwa makosa yanayohusiana na kuingia kwenye mikataba yenye mgongano wa kimaslahi.
Mhando na wasaidizi wake watatu walisimamishwa kazi na Bodi ya Wakurugenzi mnamo Julai 16, mwaka huu, kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili za ukiukwaji wa taratibu za shirika ikiwemo matumizi mabaya ya mamlaka.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Jenerali mstaafu, Robert Mboma, ilisema kuwa Mhando alisimamishwa ili kupisha uchunguzi huru na haki wa kubaini ukweli wa tuhuma hizo.
“Baada ya hapo, ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilifanya uchunguzi ili kubaini ukweli juu ya tuhuma zilizokuwa zinamkabili Mhandisi Mhando, ambapo katika uchunguzi huo, Mdhibiti aligundua kuwepo kwa ushahidi wa ukiukwaji wa taratibu za shirika na matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya Mhando,” alisema.
Mboma alisema kuwa baada ya kupokea taarifa ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za mashirika ya umma, Bodi iliteua jopo la watu watatu kusikiliza utetezi wa Mhandisi Mhando dhidi ya tuhuma mbalimbali zilizoibuliwa na mdhibiti huyo.
Kwamba baada ya kumsikiliza, jopo hilo lilimkuta Mhando na hatia dhidi ya makosa yanayohusiana na ukiukwaji wa taratibu za shirika ikiwemo mgongano wa kimaslahi.
“Pamoja na yote yaliyoelekezwa hapo juu, Oktoba 29 mwaka huu, Bodi ilikutana na kujiridhisha kuwa Mhandisi Mhando alifanya makosa yanayohusiana na kuingia kwenye mikataba yenye mgongano wa kimaslahi kinyume na taratibu za shirika. Hivyo Bodi ya Wakurugenzi iliamua kumwachisha kazi kuanzia Oktoba 29 mwaka huu,” alisema Mboma.
Wengine waliosimamishwa kazi wakati huo pamoja na Mhando ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi, Manunuzi, Harun Mattambo.
Sakata la Mhando lilizua balaa hadi bungeni kiasi cha kuwagawa wabunge katika makundi mawili, moja likimuunga mkono Waziri wa Nishati na Madini na wasaidizi wake na lingine likimtetea Mhando.
Hatua hiyo iliibua madai ya rushwa kwa baadhi ya wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini wakidaiwa kuhongwa na kampuni za mafuta ili kuikwamisha bajeti, na hivyo kumlazimu Spika wa Bunge kuivunja kamati hiyo na kuunda kamati ndogo ya uchunguzi wa tuhuma hizo.
Kamati hiyo iliyoko chini ya Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge inaongozwa na mbunge wa Mlalo, Brigedia Jenerali mstaafu, Hassan Ngwilizi na tayari imekamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti.

No comments:

Post a Comment