Thursday, November 8, 2012

Membe akalia kuti kavu Nec,achafuliwa na wanamtandao.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe akijadiliana jambo na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe walipotoka kuhudhuria kikao cha bunge, mjini Dodoma jana.

KAMPENI za kuegemea makundi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), zinazidi kukitafuna chama hicho baada ya kundi la makada wa chama hicho kumpigia kampeni chafu, mmoja wa wagombea wa Ujumbe wa Halmashauri Kuu Nec, kupitia Kapu, Bernad Membe.

Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa kundi hilo la makada linapiga kampeni ya kutaka Membe asichaguliwe katika nafasi hiyo,ili kumharibia harakati zake za kutaka kuwani urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kupitia chama hicho.

“Unajua wanachotaka kikifanya ni kumfanya ashindwe kuwa mjumbe wa Nec ili wawe na hoja ya kusema kwamba kama ameshindwa kupata hata ujumbe wa Nec atafaa kuwa rais,” alisema mmoja wa makada wa CCM waliopo mjini Dodoma kuhudhuria mkutano mkuu wa uchaguzi wa chama hicho unaoanza Novemba 10.

Kampeni zinazofanywa na kundi hilo dhidi ya Membe na watu wengine ambao hawakubaliki katika kundi hilo kwa njia ya kutoa taarifa kupitia ujumbe wa simu  na mdomo kufahamishana msimamo wao.

Membe
Hata hivyo,Membe ambaye ni pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alipotakiwa kuzungumzia suala hilo jana alisema kuwa, amepata taarifa kundi hilo kufanya kampeni chafu dhidi yake na akatangaza kiama dhidi ya wabaya wake kuwa watarajie kuona anapata ushindi wa kimbunga katika uchaguzi huo.

''Nakubaliana kabisa kwamba ziko njama za kunihujumu ambazo hata mimi nazijua, lakini wabaya wangu hao wanafanya jambo ambalo hawalijui, kwani kama wangejua wasingepoteza muda huo,'' alisema Membe.

Hata hivyo, alikataa kumtaja mtu ambaye anamhujumu, lakini akasema kuwa lipo kundi ambalo linapoteza muda wao na kuwaza habari za yeye bila ya kujua wanashindana na nguvu ya aina gani.

Waziri huyo alisema kuwa maajabu atakayoyaonyesha siku ya Novemba 13 yatakuwa ni makubwa kiasi ambacho hao waanaotaka kumhujumu watajua.

Alijifananisha na mti wa muembe ambao hutupiwa mawe wakati wote kuliko mchongoma wenye miiba ambao alisema hauwezi kutupiwa mawe kwani hauna kitu cha kuchukua juu yake.

''Kwa mfano ningeshangaa sana kama ningepita bila ya kupata misukosuko, kweli ningeshangaa sana maana nimezoea kupambana na misukosuko, lakini kitendo cha kutokea misukosuko kwangu kinadhihirisha kabisa mimi ni nani juu yao,'' alisema Membe huku akikunja ngumi kuonyesha yuko tayari kwa mpambanao huo.

Alipotakiwa kueleza kama njama hizo zinaendana na makundi ya urais alisema '' hilo mimi sijui, lakini nasisitiza kuwa njama mbaya dhidi yangu zipo na kwa vyovyote nitashinda ushindi mkubwa.''

Aliwafananisha wapinzani wake kuwa ni watu wasiokumbuka kwani walifanya hivyo hata katika uchaguzi uliopita, lakini alishinda na hata katika kipindi hiki wataaibika tena.

''Mimi niliwachapa katika kipindi kilichopita na waliaibika ndivyo ninavyowatangazia hata katika kipindi hiki kuwa ni vita takatifu, lazima nitawachapa tena kwa kichapo cha hali ya juu.'' alisema huku akionyesha kujiamini zaidi.

Kundi hilo mbali ya kupigia kampeni mbaya, Membe limetoa orodha ya wagombea ambao litawapigia kura katika nafasi ya ujumbe wa Nec.

Katika orodha hiyo yumo, Naibu waziri wa Mawasiliano, Januari Makamba ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya nje ya CCM, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Wilson Mukama, Mweka Hazina wa chama hicho, Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira na Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa chama hichjo UVCCM taifa, Martine Shigela.

Wengine ni Mbunge wa Nkenge,Asumpta Mshama, Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, David Mathayo, Jackson Msome na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na michezo, Fenella  Mukangara.

Vita kubwa inaonekana kuwa katika nafasi 10 za ujumbe wa Nec kwani mawaziri sita ni miongoini mwa wanachama 31 wa Bara watakaopamba vikali kupata nafasi hizo.

Hali ni hiyo pia kwa upande wa Zanzibar kwani katika wanachama 28 wanaowania nafasi 10 za Nec Zanzibar, wapo mawaziri wanne.

Mbali na mawaziri sita nafasi 10 za Tanzania Bara pia kuna wabunge watatu, mkuu wa wilaya mmoja na vigogo wawili wa Kamati Kuu ya chama hicho.

wa upande wa Zanzibar wamo mawaziri wanne akiwamo Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi.

No comments:

Post a Comment