Thursday, November 8, 2012

JK atoboa siri za vigogo,ni wakati wa uzinduzi wa mitambo ya gesi


Akitoa historia ya matumizi ya gesi asilia hapa nchini, Rais Kikwete alitoboa siri ya mapingamizi kutoka kwa baadhi ya vigogo serikalini kwenye harakati za kusaini mkataba wa kufua umeme.

Alisema kipindi hicho alikabiliwa na wakati mgumu baada ya vigogo hao kumkaba waziwazi na wengine kumwandikia barua ya kumtaka asianzishe mchakato wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia.

Alisema wakati huo alikuwa Waziri wa Maji na Nishati kipindi cha mwaka 1988 hadi 1994, kwenye Serikali ya Awamu ya Pili.

Rais Kikwete alisema aliandikiwa barua nyingi za kupinga matumizi ya gesi asilia ili kuzalisha umeme na badala yake wakamshauri itumike katika mradi wa kuzalisha mbolea mkoani Mtwara.

“Vigogo hao walitaka gesi hiyo itumike kuzalisha mbolea badala ya umeme. Wakaandika barua nyingi za kuupinga huo mradi (wa kuzalisha umeme) na mpaka sasa zipo wizarani... Mmeziona?” alihoji Rais Kikwete.

Aliongeza: “Vigogo hao waliamini kuwa maji peke yake yanatosha kuzalisha umeme, wakati si kweli. Mimi nilikataa na faida zake zinaonekana leo.”

Alisema kwa sasa gesi imesaidia Taifa kupunguza mgawo wa umeme kuliko vyanzo vingine vinavyotumika nchini.

Akitoa takwimu hizo, Rais Kikwete alisema katika Gridi ya Taifa, gesi inachangia asilimia 54.8 wakati maji ni asilimia 15.4 na mafuta asilimia 29.8.

Pamoja na kutoa madai hayo, Rais Kikwete hakuwataja wazi vigogo hao, lakini watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini wanaweza kuziona kwenye kumbukumbu za mafaili wizarani kwao.

Mgawo wa umeme kwisha
Rais Kikwete alisema mradi huo unaotarajiwa kumalizika mwaka 2014 utamaliza kabisa kero ya mgawo wa umeme ambayo imekuwa ikilisumbua Taifa kwa muda mrefu sasa.

Alisema mradi huo utaanza kwa kuzalisha megawati 900 na ifikapo 2015 utakuwa unazalisha megawati 3,000 na kufanya mgawo wa umeme kuwa historia.

Alisema tafiti za kitaalamu zinaonyesha kuwa kiwango cha gesi kilichopo eneo la nchi kavu kinaweza kutumika kwa miaka 90 kwa matumizi ya hapa nchini na kuuza nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment