Thursday, November 8, 2012

Matumaini ya Man City kwisha!

Roberto Mancini
Mancini amsomea mwamuzi na wasaidizi wake baada ya mechi
Meneja wa klabu ya soka ya Manchester City ya Uingereza, Roberto Mancini, amesema hana matumaini tena ya timu yake kufanya vyema katika mechi za klabu bingwa, baada ya Jumanne jioni, ikiwa katika uwanja wa nyumbani, kutoka sare ya 2-2 ilipocheza na Ajax ya Uholanzi.
City ina pointi mbili baada ya kucheza mechi nne, na lazima ishinda mechi zote mbili kujiongezea matumaini yoyote ya kuendelea mbele.
"Kwa bahati mbaya tuliondoka tu na pointi moja, na nadhani hatuna tena matumaini ya kuendelea na ligi ya klabu bingwa," alisema Mancini.
Mancini, ambaye ni raia wa Italia, aligombana na waamuzi baada ya kipenga cha mwisho, kufuatia kuamini kwamba timu yake ilinyimwa ushindi.
Sergio Aguero, baada ya kupokea mpira kutoka kwa Aleksandar Kolarov, alifunga bao la tatu, lakini msaidizi wa mwamuzi aliinua kibendera kwamba alikuwa ameotea.
Mabao ya City yalipatikana kwa juhudi kubwa, baada ya kulemewa awali magoli 2-0.
"Lilikuwa ni bao," alilalamika Mancini.
"Mwamuzi na wasaidizi wake hawakufaa. Nilimzungumzia mwamuzi, na kumwambia 'pongezi - hilo lilikuwa ni bao'.
"Mimi sitakuwa wa kwanza wala wa mwisho kumzungumzia. Katika soka hilo hutokea."
Baada ya kuingia uwanjani kumsomea mwamuzi Peter Rasmussen, Mancini alielekea kupandwa na gadhabu, huku mpiga picha akimfuata baada ya kipenga cha mwisho.
Mancini alielezea: "Mpiga picha wa video alinifuata kunipiga picha uwanjani.
"Sio filamu juu yangu, ndio hali ya mchezo. Nilimuelezea mpira umekwisha."
Licha ya malalamiko yake dhidi ya waamuzi, Mancini alikiri kwamba upungufu fulani wa timu yake ulisababisha hali hiyo ya kushindwa.
Man City walishindwa kuimarisha ulinzi wao wakati wa kona kupigwa, na kumwezesha nahodha wa Ajax, Siem de Jong, kuiongoza timu yake kuongoza 2-0 katika kipindi cha dakika 17 za mwanzo, kabla ya wachezaji wa City, Yaya Toure na Aguero kufanikiwa kusawazisha.
chanzo-bbc.com

No comments:

Post a Comment