Sunday, November 4, 2012

MAISHA PLUS:Washiriki walala wamesimama,Babu aitisha mkutano wa dharura,Wanaume waendelea kujipikia

MAISHA kijijini yanaendelea, ambapo juzi mshiriki Abdullah Ganiko kutoka Dar es Salaam alionekana kuwa na wakati mgumu, baada ya kushambuliwa na nge shingoni na mkononi mahali alipokuwa amelala.
Hata hivyo, muda mwingi Abdullah alionekana mwenye mawazo, kwani licha ya kutokewa na tukio hilo, pia hakuweza kulala kutokana na nyumba yake kuwa miongoni mwa zilizoathiriwa na mvua kijijini hapo.
Mbali na Abdullah, nyumba ya Rashid nayo ilivuja na nguo zake zililowa, jambo lililomfanya kwenda kumhadithia Babu.
Washiriki walala wamesimama
KUNYESHA kwa mvua usiku wa kuamkia juzi, kulisababisha washiriki Dora, Nell na Mage kulala wamesimama.
Washiriki hao wa kike, walilala huku wamesimama kutokana na nyumba yao kuvuja sana, lakini mwisho Mage alisema, alijitahidi kupambana na mvua lakini ilishindikana na aliloa kichwani.
Babu aitisha mkutano wa dharura
JUZI jioni, Babu aliitisha kikao na wanakijiji huku agenda kubwa ikiwa ni kujihadhari na mvua zinazoanza kunyesha kijijini.
Babu alitoa tahadhari kwa wanakijiji, ambao vyoo vyao havijazibwa juu na kuwataka kuezeka. Pia mitaro ya maji izibuliwe.
Aidha serikali ya kijiji ihakikishe inapita nyumba hadi nyumba ili kuzifanyia marekebisho zinazovuja.
SIDO yawapa changamoto washiriki
UGENI kutoka Shirika Linalohudumia Wafanyabishara Wadogowadogo (SIDO), ulitinga kijijini na kuzungumza na wanakijiji wa Maisha Plus namna ya kuwa wabunifu.
Wanakijiji hao, waliambiwa kwamba kama mtu unataka kuwa mbunifu, unapaswa kufikiria kile unachotaka kubuni wakati wa usiku ukiwa unalala, kwani muda huo unakuwa huna pilikapilika zozote.
Wanakijiji hao ambao walionekana kuvutiwa na mazungumzo hayo, walioneshwa bidhaa mbalimbali zilizotengenezwa na wajasiriamali waliokwenda kujiunga SIDO.
Wanaume waendelea kujipikia
KATIKA hali inayoonekana kubana matumizi, washiriki wa kiume wanaendelea na mchakato wa kujipikia chakula, ili kuokoa fedha walizokuwa wananunua chakula kwa mama lishe.
Wanaume hao ambao walionekana kusonga ugali, mchuzi wa dagaa uliopikwa na Justin Bayo kutokana na mchuuzi wa maembe uliopikwa na Bahati Kisura.
Wanakijiji hao wa kiume, walishtushwa na wanawake kuonekana kumiliki fedha nyingi zaidi hao.
Hatua hiyo ya kujipikia, kwa sasa inaonekana kuwapa wakati mgumu wanakijiji wanawake, ambao walitegemea kupika chakula ili kuzidi kujipatia kipato, lakini kwa sasa wateja ndio hao wameanza kukimbia.

No comments:

Post a Comment