Sunday, November 4, 2012

HATIMAYE mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Yanga, wamewashusha rasmi watani zao Simba katika kilele cha Ligi Kuu Bara

 Simba washangaa bwawa Mindu Moro, Kaseja aangua kilio
HATIMAYE mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Yanga, wamewashusha rasmi watani zao Simba katika kilele cha Ligi Kuu Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, jana.
Wakati Yanga wakichanua, upande wa pili, Simba hali ilikuwa tete kwenye Uwanja wa Jamhuri Mji Kasoro Bahari ambako walilishangaa bwawa la Mindu na kujikuta wakilala kwa mabao 2-0.
Yanga walianza pambano kwa uchu, ambako iliwachukua dakika 8 tu kujipatia bao la kwanza lililofungwa na Didier Kavumbagu, akimalizia pasi ya Mbuyu Twite, baada ya mabeki kujichanganya na kipa wao.
Bao hilo la mapema, lilionekana kuwachanganya Azam na kuwafanya kushindwa kufika langoni mwa wapinzani wao mara kwa mara. Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa bao hilo moja.
Kipindi cha pili, Yanga waliendelea kutakata na dakika ya 68, Hamis Kiiza alipachika bao la pili akiitendea haki krosi ya Athumani Idi ‘Chuji’, ambako kwa furaha alishangilia kwa kuvua jezi, kitendo kilichosababisha alimwe kadi ya njano.
Kiiza alivua jezi yake na kukimbilia kwa mashabiki wa Simba na kuwaonesha fulana yake ya ndani iliyokuwa imeandikwa; ‘Rip Mafisango rest in peace my bro’.
Patrick Mafisango, alikuwa kiungo mahiri wa Simba raia wa Rwanda mwenye asili ya DR Congo, ambaye alifariki dunia kwa ajali ya gari Mei mwaka huu, maeneo ya Veta, Chang’ombe, jijini Dr es Salaam.
Mjini Morogoro, mchezo ulitawaliwa na rabsha za mara kwa mara kutoka kwa mashabiki wa Simba waliokuwa na hasira wakidai mwamuzi Judith Gamba, alikuwa hawatendei haki.
Mtibwa ilijipatia bao dakika ya 34, lililofungwa na Mohamed Mkopi baada ya kipa Juma Kaseja kutema shuti kali la Vicent Barnabas.
Dakika ya 87, mshambuliaji mahiri Hussein Javu, aliipatia Mtibwa bao la pili, baada ya Kaseja kufanya mbwembwe langoni mwake.
Baada ya mchezo kumalizika, Kaseja aliangua kilio uwanjani huku mashabiki wakimzonga.
Aidha, wachezaji wa Simba waligoma kupanda basi lao, ambako baadhi ya viongozi wao walifanya kazi ya ziada kuwabembeleza, ambako walikubali kwa shingo upande, lakini baada ya muda Mrisho Ngasa alishuka akiwa kabadilisha nguo na kuondoka kivyake, huku akisindikizwa na mashabiki lukuki.
Kwa matokeo hayo, Yanga imekamata usukani rasmi ikiwa na pointi 26, huku Simba ikibaki na pointi zake 23, wote wakiwa na michezo 12 huku Azam ikiwa nafasi ya tatu kwa pointi 21; Mtibwa ikifikisha pointi 13.
Yanga: Ally Mustafa Barthez, Mbuyi Twite, Oscar Joshua, Naroub Cannavaro, Kelvin Yondani, Athuman Idd, Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza na Haruna Niyonzima.
Azam: Mwadini Ali, Erasto Nyoni, Ibrahim Shikanda, Aggrey Morris, Said Morad, Kipre Balou, Salum Abubakar, Jabir Aziz, John Boko, Kipre Tchetche, Hamis Mcha ‘Viali’.

No comments:

Post a Comment