Sunday, November 4, 2012

5Walioingia fainali ya EBSS hawa hapa.aka Top FIVE,ndugu wawili wang'ara

WASHIRIKI watano watakaoshiriki fainali za shindano la Epiq Bongo Star Search (EBSS), Jumamosi kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee wamepatikana.
Kupatikana kwa wakali hao ni kutokana na mchujo wa mwisho uliofanyika jana, ambapo washiriki machachari, Geofrey Kato na Husna Nassoro walitolewa.
Washiriki walioingia fainali hizo na kujikuta wakiwa katika presha ya kuwania kitita cha sh milioni 50 na mkataba wa kurekodi nyimbo zao, kutoka kampuni ya Zantel ni Nshoma Ng’hangasamala (EBSS07), Walter Chilambo (EBSS12), Wababa Mtuka (EBSS11), Nsami Nkwabi (EBSS06) na Salma Abushiri (EBSS09).
Nshoma, ambaye ni mkali wa nyimbo za asili, anatarajiwa kutoa upinzani mkali, pia huku Chilambo akiwa ni ‘noma’ kwa nyimbo laini na kuweza kupatia sauti za wasanii anaoimba nyimbo zao, huku Nsami akiwa na uwezo wa kuuchukua wimbo wa msanii na kuufanya wa kwake na kutoa burudani safi.
Msanii Wababa ni mshiriki ambaye ameonekana kuwa na mashabiki lukuki, kwani mbali na kuwa na muonekano wa kisanii, lakini pia ni mshiriki ambaye anaweza pia kulitumia jukwaa vema, wakati Salma ana sifa za kuimba na kutumia gitaa tofauti na washiriki wenzake wote.
Kinyang’anyiro hicho kitasindikizwa na wasanii mbalimbali wa hapa nchini kama vile Rich Mavoko, Omi Dimpoz, Ben Paul, Lina, Amini, Mzee Yusuf, Haji Ramadhan, Mwasiti, Ditto, Laila Rashid, Linex na Barnaba.
Akizungumzia shindano hilo, Jaji Mkuu wa EBSS 2012, Ritha Paulsen, alisema kuwa maandalizi ya fainali yamekamilika na kuwaomba Watanzania wengi wajitokeze kutazama fainali hizo kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee.
Akizungumzia zaidi fainali hizo, Madam Ritha alisema shindano bado halijafungwa, kwani wapenzi wa shindano hilo wanatakiwa kuendelea kumpigia kura mshiriki anayempenda ili aibuke mshindi.
Kwa upande wake, Ofisa Biashara Mkuu wa Zantel, Sajid Khan, alisisitiza umuhimu wa Watanzania kumpa ushirikiano mshindi, hasa kutokana na shindano hili kuamuliwa kwa kura zao.
Tiketi za shindano hilo zimeanza kuuzwa katika maeneo tofauti kwa sh 70,000, sh 30,000 pamoja na sh 10,000 viti vya kawaida.

No comments:

Post a Comment