Katika kuendeleza azma yake ya kuwawezesha wananchi kubadili maisha
kupitia teknolojia ya simu za mkononi, Kampuni ya Vodacom Tanzania, sasa
inawawezesha wateja wake kutumia huduma ya M-pesa kwa faida zaidi
katika kila muamala wa utumaji wa pesa.
Kupitia uwezeshaji huo,
mteja wa Vodacom anayetuma pesa kwa njia ya M-pesa, atapokea muda wa
hewani bure ukiwa na thamani sawa na gharama alizotozwa wakati akituma
pesa hizo, kwenda sehemu yoyote nchini.
Huduma hiyo itatolewa mara baada ya mteja kumaliza kutuma pesa hizo.
Akizungumzia
mpango huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Rene Meza, alisema
hiyo ni moja ya njia za kuwashukuru wateja zaidi milioni 4.5
wanaoendelea kuiamini huduma ya M-pesa na kuitumia kila siku katika
shughuli zao.
“Mteja haitaji kujisajili ili kunufaika na
kampeni hii na wala hatotumia muda kupokea muda wa hewani wa bure,
Vodacom itampatia shukrani yake ya muda wa hewani kwa kutumia M-pesa
mara tu atakapomaliza kutuma fedha hizo kwenda kwa mteja wa Vodacom
katika sehemu yoyote hapa nchini,” alisema Meza.
Alisema chini ya
mpango huo, wateja wa Vodacom wanapata zaidi cha kujivunia katika
huduma yao ya M-pesa huku wakiwa na wigo mpana zaidi wa kufurahia
mawasiliano kupitia mtandao wa Vodacom kwa kuwa na salio la ziada la
kufanya hivyo.
“Ni fursa nyengine kwa wateja wetu kufurahia kila
watumapo pesa kwa M-pesa huku wakipata cha ziada kufurahia kuwa wateja
wa Vodacom kwa kuongea zaidi miongoni mwao,”alisisitiza.
Tangu
ilipoanzishwa Aprili mwaka 2008 huduma ya M-pesa imebakia kuwa huduma
bora, salama, ya uhakika na yenye kuaminika kwa Watanzania.
No comments:
Post a Comment