Wednesday, November 7, 2012

Azam kupigilia msumari mwingine kwa Simba leo?

 
BAADA ya kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Yanga, timu ya Azam FC leo itashuka dimbani kuivaa JKT Oljoro ikiwa na lengo la kupata ushindi na kuiporomosha Simba hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na wenyewe kukamata nafasi ya pili.

Washindi hao wa pili msimu uliopita wenye pointi 21 hivi sasa watakuwa kwenye uwanja wao wa Azam Complex, Chamazi wakiwakaribisha Oljoro, ambapo wakishinda watafikisha pointi 24 na hivyo kuizidi Simba kwa pointi moja kabla ya mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu mwishoni mwa wiki.

Pia ushindi huo utaisadia Azam kupunguza pengo kati yake na vinara wa ligi hiyo Yanga wanaoongoza msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 26.

Kama haitoshi, Azam inahitaji kushinda mechi ya leo ili kuwathibitishia mashabiki wake kwamba ilikuwa sahihi kufanya mabadiliko katika benchi lake la ufundi ilipomtimua Boris Bunjak na kumrejesha kocha Stewart Hall.

Nayo JKT Oljoro yenye pointi 14 iliyotikisika katika mechi zake za hivi karibuni kwa vyovyote vile haitakubali kuwa ngazi ya kuipandisha Azam zaidi ya kupigania hadhi yake kwa kusaka ushindi utakaoirudisha katika nafasi za juu.

Mechi nyingine ya Ligi Kuu itakuwa Morogoro, ambapo Mtibwa Sugar iliyochumpa hadi nafasi ya sita baada ya kuikandamiza Simba mabao 2-0 na kufikisha pointi 16 kwenye uwanja wa Jamhuri, itarudi nyumbani maeneo ya Manungu Turiani na kuumana na JKT Ruvu inayokamata nafasi ya 10 ikiwa na pointi 14.

Pia Coastal Union inayoshika nafasi ya nne ikiwa na pointi 19, itakabana koo na wachovu  Polisi Morogoro wanaokamata mkia wakiwa na pointi tatu katika pambano litakalofuka moshi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Wakati huohuo; Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeifanyia  marekebisho ratiba ya Ligi Kuu, ambapo baadhi ya michezo iliyokuwa ichezwe Novemba 11 imehamishiwa Novemba 10.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema jana kuwa mchezo pekee utakaofanyika Novemba 11 ni kati ya Yanga na Coastal utakaofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani.

Alisema kuwa marekesho hayo yamefanyika ili kutoa nafasi kwa kikosi cha timu ya Taifa 'Taifa Stars' ambacho kitatangazwa kesho kupata muda wa kujiandaa na mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayofanyika Novemba 14 kwa mujibu wa kalenda ya Shirkisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

"Kocha Kim anahitaji angalau siku mbili za maandalizi ya timu yake, kufuatia ombi hilo tuliamua kuzungumza na Kamati ya Ligi ambayo ilikubali kufanya mabadiriko,"alisema Osiah.

Alisema,"hivi sasa tupo katika mawasiliano ya mwisho na baadhi ya nchi ili kujua ni ipi itakayocheza na Stars mambo yatakapokuwa tayari tutaweka wazi."

No comments:

Post a Comment