Wednesday, November 7, 2012

Apendekeza magari 10 tu msafara wa Rais,Mtwara wataka Rais aongezewe madaraka

WAKAZI wa Kijiji cha Msijute, Halmashauri ya Wilaya Mtwara, mkoani hapa wametaka katika Katiba ijayo, Rais aongezewe madaraka ili kumpa nguvu ya kufanya uamuzi.
Wakitoa maoni yao mbele ya Tume ya kukusanya maoni ya Katiba, wakazi hao bila kufafanua aina ya madaraka anayopaswa kuongezewa Rais,  walisema hawaoni umuhimu wa kupunguza madaraka ya kiongozi huyo wa juu wa nchi.

Saidi Nawanda (62) na Selemani Likoko (68) kwa nyakati tofauti walisema mamlaka aliyonayo Rais kwa sasa hayatoshi hivyo ni muhimu aongezewe.
“Rais aongezewe madaraka, ili akisema jambo basi litekelezwe” alisema Nawanda bila ya kufafanua madaraka anayopaswa kuongezewa.

Maoni kama hayo pia yalitolewa na Likoko, ambaye alihoji iweje Rais apunguziwe madaraka badala ya kuongezewa.“Rais aongezewe madaraka, na kamwe asipunguziwe” alisema Likoko.

Katika mkutano huo ulioendeshwa na mwenyekiti  wa timu iliyopo hapa, Sengondo Mvungi, ulitanguliwa na maelezo ya umuhimu wa kutoa maoni ya Katiba yaliyotolewa na Mjumbe wa Tume hiyo, Kibibi Hassan ambaye aliwaambia ni wakati mwafaka kwao kutengeneza Katiba waitakayo.

“Tumieni fursa hii kutoa maoni yenu, jisikieni huru, utakachosema ndicho kitakachonukuliwa, baada ya hapa tutarudi kwenu tukiwa na rasimu ya Katiba, safari hiyo tutaiwasilisha kwenu kupitia mabaraza ya wilaya” alisema Hassan.

Aliongeza kuwa “Tutaipeleka kwenye Bunge maalumu la Katiba na baada ya hapo italetwa kwenu kwa ajili ya kupigia kura ya ndiyo na hapana, msiwe na wasiwasi, hii ni Katiba yenu.”
 MKAZI wa Kata ya Kintinku, Wilaya ya Manyoni, Hadija Ismail (58) amependekeza Katiba Mpya iwe na kifungu kinachosema misafara yote ya viongozi hususan Rais  iwe na magari yasiyozidi  10 ili kupunguza gharama za uendeshaji.

 Hadija alisema kuwa fedha zinazotumika kugharimia magari zaidi ya 30 yanayokuwa katika msafara mmoja wa Rais, zinaweza kujenga madarasa na kuwalipa fedha ya ziada walimu wanaoishi vijijini.


Akizungumza wakati akitoa maoni juu ya Katiba Mpya juzi, Hadija alisema  Katiba Mpya inatakiwa kueleza wazi suala hilo, kwa kuwa fedha za walipa kodi ndiyo zinazotumika kuendeshea magari hayo.
“Rais msafara wake unatakiwa kuwa na magari 10 tu, msafara wa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais unatakiwa kuwa na magari matano matano,” alisema Hadija.
Alisema kuwa ni ajabu kwa viongozi wa Serikali kutumia magari mengi katika shughuli zao za kila siku wakati kuna baadhi ya vijiji, wananchi wanatumia jembe la mkono katika shughuli za kilimo.

“Mfano msafara mmoja unakuwa na magari 30, ukipiga hesabu ya gharama ya mafuta kwa magari 20, labda kutoka Dodoma mpaka Singida, zinatosha kabisa kununulia trekta la kilimo” alisema Hadija.
Pia Hadija alisema kuwa viongozi wote wanaochaguliwa na wananchi wanatakiwa kukaa madarakani kwa vipindi viwili tu na siyo kama ilivyo sasa ambapo wapo wabunge wenye miaka zaidi ya 30 bungeni.
“Diwani na mbunge nao wanatakiwa kuwa na vipindi viwili tu vya kugombea kama ilivyo kwa Rais” alisema.

No comments:

Post a Comment