Sunday, November 4, 2012

Kutimuliwa na kurejeshwa Stewart uwe mwanzo mpya

MICHUANO ya 39 ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) maarufu kama Kombe la Kagame iliyofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 14 hadi 28, iliisha kwa Yanga kutwaa ubingwa ikiwa ni mara ya nne kwao, ikifanya hivyo pia miaka ya 1975, 1993 na 1999.
Ingawa Yanga ilitwaa ubingwa huo kwa kuwafunga Azam 2-0 katika fainali iliyochezwa Julai 28, Azam inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini Saidi Salim Bakhressa, ilistahili pongezi kubwa kwa kufika hatua hiyo licha ya kushiriki kwa mara ya kwanza.
Kilichovutia kwa Azam sio tu kufika fainali, bali kucheza soka ya kiwango cha juu kuanzia mechi ya ufunguzi hadi ya fainali.
Pamoja na hayo, katika hali isiyotarajiwa na wengi hasa kwa wenye kuitakia mema soka ya nchi hii, aliyekuwa kocha wake, Mwingereza Stewart Hall alitimuliwa.
Kwa mujibu wa uongozi wa Azam, ulifanya hivyo kwa kuchukizwa na kitendo cha Stewart kumpanga Mrisho Ngasa katika mechi ya fainali dhidi ya Yanga.
Uongozi ukiona kwamba nyota huyo hakustahili kucheza kutokana na kuonyesha mapenzi ya wazi kwa timu yake ya zamani ya Yanga katika mechi ya nusu fainali ya michuano hiyo.
Katika mechi hiyo ambayo iliihusisha Azam na AS Vita ya DR Congo, Ngasa alishangilia ushindi kwa kuvaa jezi ya Yanga aliyowahi kuichezea kabla ya kujiunga na Azam msimu wa 2009/10.
Furaha ya Ngasa haikuwa tu ushindi wa timu yake hivyo kutinga fainali, pia alikuwa kati ya wafungaji hivyo timu hiyo kuvuna ushindi wa mabao 2-1.
Zaidi ya hapo, furaha yake ilikolezwa pia na kufunga bao hilo akiingia kutokea benchi kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche, hivyo kwa namna fulani ilikuwa ni kufikisha ujumbe kwa Stewart na benchi la ufundi.
Kitendo hicho kiliwakera viongozi wa Azam hadi kutaka kumwadhibu baada ya kwisha kwa michuano hiyo.
Kabla ya kumwadhibu, wakamtaka Stewart kutompanga kwenye mechi ya fainali dhidi ya Yanga iliyochezwa Julai 28, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Hoja ya uongozi wa Azam ni kwamba kitendo cha Ngasa kiliidhalilisha nembo ya klabu hiyo ambayo ilifanya kazi kubwa kuijenga.
Zaidi ya hilo, viongozi wa Azam wakaona kuwa kwa vile Ngasa alionyesha mapenzi ya dhati kwa Yanga aliyowahi kuichezea kabla ya kuihama msimu wa 2009/10, angeweza kucheza kuihujumu timu yao kwa kucheza chini ya kiwango.
Iwe kwa kutii maelekezo au vinginevyo, Stewart hakumwanzisha Ngasa katika mechi ile hadi kipindi cha pili, wakati huo timu yake ikiwa nyuma kwa mabao 2-0.
Baada ya mechi hiyo iliyokwisha kwa Yanga kushinda na kutwaa ubingwa, uongozi wa Azam ukamfukuza Stewart, licha ya kuipatia mafanikio makubwa kwa kipindi alichodumu nayo akiiwezesha kushika nafasi ya tatu msimu wa 2010/11 kabla ya kukamata nafasi ya pili msimu wa 2011/12.
Kwa kukamata nafasi ya pili msimu uliopita nyuma ya Simba na mbele ya Yanga, msimu huu Azam itashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho huku Simba ikicheza michuano ya Ligi ya Mabingwa.
Tutaendelea
chanzo- Deodatus Mkuchu

No comments:

Post a Comment