Sunday, November 4, 2012

Hatimaye Yanga kumlipa aliyekuwa mchezaji wake, John Njoroge, kiasi cha sh mil 17.

Yanga iliamriwa kumlipa kiasi hicho kutokana na hatua yake ya kukatisha mkataba baina yake na nyota huyo kwenye msimu wa 2008/9.
Huo ni uamuzi uliofikiwa Januari mwaka huu na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kupitia Kitengo chake cha Usuluhishi wa Migogoro (DRC).
Katika barua ya Fifa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kama Yanga ingeshindwa kulipa deni hilo kwa wakati, ingeweza kukumbana na adhabu kali ikiwemo kushushwa daraja.
Zaidi ya hapo, Yanga pia ingenyang’anywa pointi kwa kiwango ambacho kingetajwa na Fifa; kupigwa faini au adhabu zote kwenda kwa pamoja.
TFF ambao ni wasimamizi wa maendeleo ya mchezo wa soka, wakaisihi Yanga kutekeleza hukumu hiyo kuepuka adhabu ambayo ingetolewa na Fifa.
Sisi Tanzania Daima tukiwa sehemu ya wadau wa michezo na maendeleo kwa ujumla, tulitimiza wajibu wetu kwa kuwasihi Yanga kufanya kila wawezalo kuhakikisha wanamalizana na Njoroge.
Kwa uzito ule ule ambao tuliitumia kuisihi Yanga kufanya hicho ili kutoadhibiwa na Fifa, pia tunaandika kwa mara nyingine, safari hii tukiwapongeza kwa kumaliza jambo hilo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Lawrance Mwalusako, tayari wameshamalizana na nyota huyo kwa kumtumia fedha zake zote, hivyo wapo huru katika hilo.
Tunawapongeza Yanga kwa sababu kama wangeshindwa kutekeleza hukumu hiyo, ni wazi ingeadhibiwa vikali ikiwemo kushushwa daraja, hivyo kuathiri mustakabali wao na soka ya Tanzania kwa ujumla.
Tunasema hili kutokana na ukweli kuwa, Yanga ni moja ya klabu kongwe na maarufu nchini kama ilivyo Simba, hivyo kitendo cha kushushwa daraja, kingekuwa pigo kubwa kwa soka yetu.
Pamoja na kuwapongeza viongozi wa Yanga kwa hili la Njoroge, pia ni wakati sasa kwao kujifunza kutokana na makosa kwani kama si kukatisha kihuni mkataba wake, matatizo haya yasingetokea.
Aidha, busara ya uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti wake Yusuf Manji ya kumlipa Njoroge fedha zake, iwaongoze pia kuona haja ya kuyashughulikia kikamilifu madai ya aliyekuwa Kocha wao, Mserbia Kostadin Papic.
Tunashauri hili kwa kuzingatia kuwa, kitendo cha wachezaji na makocha kwenda Fifa kuzishitaki klabu zetu, si matope kwa klabu husika tu, bali kwa soka ya nchi yetu.
Kama sifa hiyo mbaya itaenea kote duniani hasa kutokana na mazingira ya sasa ya teknolojia ya mawasiliano, ni wazi makocha na wachezaji watasita kuja nchini na kuingia mikataba. Tusifike huko.
Tunamaliza kwa kuwapongeza Yanga kwa kumalizana na Njoroge kuhusu deni lake, pia klabu hiyo na nyinginezo nchini, zichukulie hilo kama funzo kwao.

No comments:

Post a Comment