Sunday, November 4, 2012

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad,Angurumu Zanzibar

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ameelezea kuchukizwa na vitendo vya unyanyasaji wa raia wasio na hatia vilivyofanywa na Jeshi la Polisi likishirikiana na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Seif alitoa kauli hiyo juzi wakati akihutubia mamia ya wafuasi wa chama hicho katika viwanja vya Demokrasi, Kibanda maiti mjini Zanzibar, huku akivilaumu vyombo vya dola kwa kutochukua hatua stahiki kudhibiti vitendo hivyo.
Alisema hatua zilizochukuliwa katika kurejesha amani baada ya kutokea kwa vurugu hazikuwa sahihi kwani zimekuwa zikiwadhalilisha na kuwanyanyasa wananchi wasiokuwa na hatia pamoja na kuhujumu mali zao.
Seif amabye pia ni Makamu wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliongeza kuwa amechukizwa pia na tukio la kuuawa kwa askari polisi, Koplo Said Abdulrahmani, katika eneo la Bububu.
Alisema kuwa bado serikali na vyombo vya dola vina jukumu la kulinda haki za raia kwa kuwasaka wanaohusika na tukio hilo badala ya kuwanyanyasa raia wasiokuwa na hatia.
“Sikufikiria kama vitendo hivi vingetokea Zanzibar katika wakati huu wa kutekeleza maridhiano ndani ya serikali ya umoja wa kitaifa,” alisema.
Hata hivyo, alitahadharisha kuwa huenda vitendo hivyo vimepangwa kuvuruga umoja wa Wazanzibari, ambao umeiletea sifa kubwa Zanzibar, na kuwataka wananchi kutokubali kuingizwa katika mtego huo wa kuvunjika kwa umoja na mshikamano wao.
Maalim Seif alibainisha kuwa, vikundi vinavyolalamikiwa kufanya vurugu vikiwemo vya Ubaya Ubaya, Mbwa Mwitu na Janjaweed vilikuwepo kabla ya tukio hilo na kwamba vimetokana na kundi kubwa la vijana lililoahidiwa kupewa ajira baada ya uchaguzi.
Katika hatua nyingine, Seif aliitaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba kufanya kazi kwa uadilifu na kuheshimu mawazo ya wananchi wanayoyatoa bila ya kuonyesha upendeleo kwa baadhi ya watu au makundi fulani.
Alisema tume hiyo inaonekana kuanza kuwa na upendeleo kwa baadhi ya watu na makundi fulani, hivyo ni vyema mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba akatambua kuwa wanalazimika kuheshimu mawazo ya wananchi wote.

No comments:

Post a Comment