Sunday, November 4, 2012

Kanuni za maadili zawachanganya Wabunge

SUALA la Bunge kuandaa kanuni za maadili ili kuwadhibiti wabunge ambao wanatumia mianya ya kanuni zilizopo kufanya makosa mbalimbali ikiwamo kujihusisha na vitendo vya rushwa,limechukua sura mpya baada ya wabunge kueleza kuwa haziwezi kusaidia kuwabadilisha tabia wabunge.
Wiki iliyopita, Mwananchi ilibaini kuwapo kwa mpango wa kuandaliwa kwa kanuni za maadili ili kuwadhibiti wabunge ambao wanatumia mianya ya kanuni zilizopo kufanya makosa mbalimbali ikiwamo kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel zinaeleza kuwa hatua hiyo ya Bunge inatokana na wabunge kutuhumiwa kwa makosa mbalimbali wanayoyafanya wakiwa nje ya ndani ya Bunge ikiwamo rushwa.
Joel alisema masharti hayo mpaka sasa yapo katika hatua ya kuchapwa na kwamba muda si mrefu kanuni itatoka.
Alisema wamegundua kuwa baadhi ya wabunge watumia Kanuni za Bunge zilizopo kuzikwepa na kufanya mambo yasiyofaa ambayo yanashusha hadhi ya Bunge.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofuati katika Viwanja vya Bunge mjini Dodoma, wabunge hao wameshauri wabunge wenyewe kujitambua kuwa wao ni kioo cha jamii.
Mbunge wa Mbeya mjini, Chadema, Joseph Mbilinyi alisema  kanuni za maadili kwa ajili ya wabunge ambazo zinaandaliwa haziwezi kuwabadilisha tabia wabunge.
Alisema sheria na kanuni za kumzuia mbunge kufanya mambo yasiyofaa zipo, lakini bado wanaendelea kuvivunja na baadhi hawachukuliwi hatua.
Mbilinyi alisema wananchi wanataka kuona watu wanaotuhumiwa kwa rushwa wakiwamo wabunge wanachukuliwa hatua kwa kutumia sheria zilizopo.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, CCM, Ali Kessy alisema kuwa kanuni hizo haziwezi kusaidia badala yake vyombo vya dola ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), zifanye kazi yake bila ya upendeleo.
Alishauri wabunge wabadilishe tabia zao kwa kuacha kujiingiza katika vitendo vya kuvunja sheria kwani wao wajitambue kuwa ni vioo cha jamii.
Kwa upande wake, Mbunge wa Mkanyageni, CUF, Mohammed Mnyaa alisema kutungwa kwa kanuni za maadili kwa wabunge kutasaidia kuwadhibiti wabunge ambao wanafanya mambo yanayoshusha heshima ya wabunge.
Alisema kanuni hizo zitasaidia kuleta ustarabu miongoni mwa wabunge, kwani kila wanapotaka kufanya mambo yasiyofaa watakumbuka adhabu ambayo wataipata kutokana na kitendo hicho.
“Kuwapo kwa kanuni za maadili kutasaidia wabunge kujiheshimu. Kwa mfano Wabunge kuonekana baa wakifanya mambo yasiyofaa sasa kutapungua,” alisema.
Mbunge wa Iringa mjini, Chadema,  Peter Msigwa alisema tatizo la kuvunja sheria ikiwamo kupokea au kutoa rushwa sio la wabunge pekee nchi hii.
Alisema sheria zilizopo zinatosheleza sana kudhibiti watu kufanya mambo yasiyofaa ikiwamo rushwa, lakini viongozi wameshindwa kuzissimamia.Mbunge huyo alisema kuwa na sheria nyingi sio kumaliza tatizo, bali kinachotakiwa ni kuhakikisha watuhumiwa wanachukuliwa hatua zinazostahili.

No comments:

Post a Comment