Sunday, November 4, 2012

TETEMEKO limeendelea kulikumba Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kutokana na mamia ya wafanyakazi wa shirika hilo kupanguliwa kama hatua ya kuvunja mtandao wa wizi na hujuma ndani yake.




Habari ambazochanzo hiki kilizipata na kuthibitishwa na uongozi wa juu wa Tanesco zinasema hadi sasa wafanyakazi 190 wa Tanesco wameshakabidhiwa barua za kuhamishwa na nusu ya watumishi hao ni katika Mkoa wa Dar es Salaam pekee.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, wafanyakazi 95 wamepanguliwa kutoka katika mikoa ya Tanesco iliyopo katika Jiji la Dar es Salaam pekee na wamehamishiwa mikoani ambako wanatakiwa wawe wameripoti katika vituo vyao vipya vya kazi ifikapo Novemba 15, mwaka huu.

Kadhalika idadi kama hiyo ya watumishi kutoka mikoani wamehamishiwa Dar es Salaam, hatua ambayo inalenga kuimarisha utendaji katika jiji hilo ambalo licha ya kuwa kitovu cha uchumi wa nchi, huduma za Tanesco zimekuwa zikilalamikiwa kuwa haziridhishi.

Hatua hiyo ya kupangua wafanyakazi hasa wa Dar es Salaam, imekuja siku chache tangu Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco ilipomwachisha kazi rasmi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, William Mhando kutokana na ukiukwaji wa maadili ya uongozi.

Kadhalika tayari Tanesco imeshawafukuza kazi wafanyakazi wake 29 waliothibitika kufanya makosa ya wizi wa fedha za shirika na hujuma katika miundombinu ya umeme, huku wafanyakazi wengine 19 wakiwa wamesimamishwa kazi wakati uchunguzi wa tuhuma zao ukiwa bado unaendelea.

Wafanyakazi waliosimamishwa ni tofauti na vigogo waliosimamishwa pamoja na Mhando ambao pia hatima yao inaweza kujulikana wiki hii, baada ya uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili kukamilika.

Hao ni pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji Huduma za Shirika, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na Meneja Mwandamizi Ununuzi, Harun Mattambo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchem Mramba akizungumza na gazeti hili, alikiri kuwapo kwa uhamisho wa wafanyakazi hao na kwamba huo ni utaratibu wa kawaida wa shirika.

“Ni kweli kwamba tunafanya marekebisho ya utendaji wetu wa ndani, ni suala la kawaida tu, kwani kuna ajabu gani kuwahamisha watu? Tunaimarisha utendaji wetu, kwa hiyo mimi sidhani kama hilo ni jambo kubwa,” alisema Mramba na kuongeza:

“Nadhani ninyi mnafahamu kwamba tuna changamoto ya kukabiliana na malalamiko ya wateja wetu, tunatakiwa kutoa huduma kukidhi mahitaji yao, kwa hiyo tunajitizama hapa na pale, ili kuona kama tunaweza kuimarisha utendaji na kukidhi matakwa ya tunaowapa huduma.”
chanzo-mwananchi

No comments:

Post a Comment