Sunday, November 4, 2012

Kibano cha Pinda chamtikisa mkuu wa mkoa wa Kagera

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameanza kuwabana wakuu wa mikoa na kuwa yuko tayari kuwawajibisha endapo ataendelea kupokea taarifa zenye kasoro kutoka maeneo wanayosimamia.
Hayo yalibainika mwishoni mwa wiki baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera  Fabian Massawe kulicharukia Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba na watumishi,kufuatia taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali kubainisha hujuma ya miradi ya maendeleo.
Huku akisoma sehemu ya barua aliyodai imetoka katika Ofisi ya Waziri Mkuu,alisema hayuko tayari kuwajibishwa kutokana na uzembe wa watumishi na madiwani ambao wanashindwa kutekeleza wajibu wao wa kuisimamia halmashauri.
“Utawajibika kwa taarifa zenye kasoro katika mkoa wako"alinukuu sehemu ya barua hiyo na kusema hayuko  tayari kuwajibika kwa sababu ya uzembe wa madiwani na watumishi na kudai wakati mwingine madiwani huyafumbia macho madudu  yanayofanyika ndani ya halmashauri kwa sababu  pia wao  ni sehemu ya watuhumiwa.
Mkuu wa Mkoa alitumia nafasi hiyo kuishutumu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na  Rushwa(Takukuru),kwa kukaa kimya dhidi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba waliotajwa na Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali kuhusika na hujuma ya miradi ya maendeleo.
Akisoma matokeo ya ukaguzi uliofanywa na Mkaguzi Mkuu mbele ya Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo,Massawe alisema kuwa Takukuru haifanyi kazi kwani ilitakiwa kuwa imewachukulia hatua baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo.
Miongoni mwa mambo yaliyomstaajabisha Massawe ni watumishi kufanya biashara ya kuiuzia halmashauri yao mafuta,vifaa vya ofisi na kukodisha magari hali aliyosema inaleta mgongano wa maslahi na kuitaka Takukuru kuwahoji watuhumiwa.
“Takukuru hamfanyi kazi mnaacha watuhumiwa wanaendelea kuwa huru,nataka kupata matokeo ,manunuzi yanafanyika bila uwazi wa ushindani, miradi inatekelezwa chini ya kiwango, na hata baba, mama na watoto wanapewa tenda,”alisema Massawe.
Aidha alisema ukaguzi ulibaini kuwa halmashauri hiyo iko taabani huku akiwataka madiwani kuacha woga na kuwataja aliowaita mafisadi wanaotafuna fedha za halmashauri hiyo kupitia utekelezaji duni wa miradi ya maendeleo.
Pia alilitaka Baraza hilo kuwawajibisha haraka baadhi ya watumishi ambao katika ukaguzi maalumu uliofanywa na Tamisemi kwa kushirikiana na ofisi yake walibainika kuhujumu miradi ya maji, afya na elimu.

Awali, Mwenyeki wa Halmashauri hiyo, George Katomero alisema kuwa mtiririko wa mapato sio mzuri na kuwa hawana takwimu sahihi zinazowasaidia kupima kiwango wanachostahili kukusanya kila mwezi kutoka kila chanzo cha mapato.

No comments:

Post a Comment