Friday, November 9, 2012

Kampeni za Nec CCM zatinga bungeni

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David. 

JOTO la uchaguzi wa Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC), linazidi kupanda. Jana, baadhi ya wabunge walilazimika kuingia na vipeperushi vinavyoeleza wasifu wao ndani ya Ukumbi wa Bunge kiasi cha kufanya sehemu za viti wanavyotumia kujaa karatasi hizo.
Vipeperushi vilivyoonekana kutawala zaidi katika ukumbi huo ni vya Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David.
Pia jana, sehemu kubwa ya Viwanja vya Bunge ilijaa wapambe wa wagombea wengi wakiwa ni makada wa CCM kutoka Mkoa wa Dodoma.
“Tumekuja kufanya kazi bwana! We acha tupige kazi zetu si unajua msimu wa mavuno unafikia mwisho,” alisema mmoja wa wapambe wa wagombea, huku akiwa na bahasha iliyojaa vipeperushi vya ‘mgombea wake’.
Baadhi ya wabunge na mawaziri ambao wanagombea nafasi hiyo, walionekana wakihama katika viti vyao na kupita kwa wabunge watakaopiga kura au wenye nguvu kupiga kampeni.
Baada ya kuahirishwa kwa shughuli za Bunge mchana, baadhi ya wagombea walikuwa wakipita kwa wabunge mbalimbali kuomba kura na kuwapa vipeperushi.

Rushwa
Mji wa Dodoma umefurika wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, huku vitendo vya rushwa vikifanyika waziwazi.
Baadhi ya wagombea hivi sasa wanatumia wapambe wao kukutana na wajumbe mbalimbali kutoka mikoani kuwashawishi wawapigie kura wagombea wao, huku wakiwapa fedha na vinywaji.
Maeneo ambayo yanatumiwa na wapambe wa wagombea hao kukutana na wajumbe kuomba kura ni kwenye baa na hoteli walikofikia.
Mmoja wa mjumbe wa mkutano huo ambaye hakupenda kutajwa jina lake, alisema jana kuwa mgombea mmoja wa Nec alimpa Sh50,000 ili ampigie kura.
Hata hivyo, kutokana na kufuatiliwa na kuchungwa, wagombea wengi kwa nyakati za usiku hawaonekani mitaani ka kazi hiyo huwaachia wapambe wao.

No comments:

Post a Comment