RAIS Jakaya Kikwete amejikuta akipokewa na mabango wakati akizindua 
mradi mkubwa wa bomba la gesi asilia linalotoka Mtwara hadi eneo la 
Kinyerezi jijini  Dar es Salaam.
Mradi huo unatarajiwa kumaliza 
kabisa tatizo la umeme wa mgawo ifikapo mwaka 2015 kwa kuzalisha 
megawati 3,000 ambazo ni zaidi ya mahitaji ya umeme kwa sasa.
Wanaume
 wawili waliokuwa na mabango kwenye kundi la watu zaidi ya 20, 
waliyanyanyua juu mabango yanayomtaka Rais Kikwete aingilie kati malipo 
ya fidia za viwanja na mali zitakazoathirika kwenye moja ya mradi wa 
gesi eneo hilo baada ya kuzungushwa kwa muda mrefu.
Tukio hilo 
lilitokea wakati Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik akitoa 
hotuba ya kuwakaribisha wageni na kuelezea umuhimu wa mradi huo kwa 
wakazi wa Dar es Salaam.
Watu hao walinyoosha juu mabango hayo 
kuelekea jukwaa kuu, alikokuwa amekaa Rais Kikwete jambo lililosababisha
 maofisa usalama kuwaamuru washushe chini, lakini kundi hilo lilianza 
kuzomea hivyo kusababisha usikivu hafifu kwenye  mkutano huo 
uliohudhuriwa na mamia ya wananchi.
Kuona hivyo, Mkuu wa Mkoa 
alisitisha hotuba yake na kutoa ufafanuzi juu ya madai hayo akisema 
taarifa za madai yao tayari wanazo na zinashughulikiwa kuanzia leo.
Sadick
 aliwasisitizia kuwa kitendo walichokifanya wakazi hao siyo sahihi kwa 
sababu madai yao hayahusu mradi ambao unazinduliwa na Rais Kikwete bali 
kampuni binafsi ya Kilwa Energy ambayo ipo kwenye mchakato wa kuwekeza 
katika mradi wa kuzalisha umeme.
“Madai yenu tunayajua na tayari 
tumeanza kuyashughulikia, lakini mnapaswa kufahamu kuwa madai yenu 
hayahusu mradi huu ambao Mheshimiwa Rais anauzindua leo,” alisema Sadick
 na kuongeza:
“Madai yenu yanahusu mradi wa kampuni binafsi ya 
Kilwa Energy ambao bado haujasainiwa. Tumekwisha kukubaliana kesho (leo)
 tutakutana na viongozi wenu kujadili.”
Moja ya bango lilisomeka: “Mtukufu Rais tunaomba utusaidie malipo ya fidia ya viwanja vyetu maana tumezunguswa muda mrefu.”
 
 
 
 

 
No comments:
Post a Comment