Friday, November 2, 2012

Jeshi latuhumiwa na mauaji ya vijana

Jeshi la Nigeria
                                                      Jeshi la Nigeria
Raia wameiambia BBC kuwa, vijana kadhaa wameuawa kwa kupigwa na wanajeshi wa serikali mjini Maiduguri, Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo.
Imamu mmoja ameiambia BBC kuwa vijana 11 kutoka mtaa anaoishi, wameuawa vijana wanne kati yao wakiwa wanawe wa kiume.
Mauaji hayo yanayodaiwa kufanywa na wanajeshi wa serikali, yametokea ambapo shirika la kutetea haki za kibinadam la Amnesty International, limeshutumu maafisa wa ulinzi wa serikali kwa kuwanyanyasa raia wakati walipowasaka wanamgambo wa Kiislamu.
Lakini msemaji wa jeshi katika eneo hilo la Maiduguri amekanusha madai hayo na kusema hana taarifa kuhusu tukio hilo.
Hata hivyo Luteni Kanali Sagir Musa, ameiambia BBC kuwa uchunguzi utaanzishwa kufuatia madai hayo.
Maiduguri ni ngome ya wapiganaji wa Kiislamu wa Boko Haram, ambao wanapambana na jeshi la serikali wakitaka sheria za Kiislamu maarufu kama sharia kutumika nchini humo.
Mamia ya watu wameuawa katika maeneo ya Kaskazini na Kusini mwa Nigeria, katika mashambulio yanayosadikika kutekelezwa na kundi hilo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Ripoti ya shirika la Amnesty International iliyochapishwa hiyo jana, imesema kuwa wanajeshi hao wa serikali walihusika na visa vingi vya ukiukwaji wa haki za kibinadam, wakati wa operesheni zao za kuthibiti wapiganaji hao wa Boko Haram.
Malam Aji Mustapha, ambaye ni Imamu katika msikiti mmoja mjini Maiduguri, amesema, baada ya maombi ya Alhamisi asubuhi, wanajeshi walimkamata na kumpeleka pamoja na watoto wake hadi uwanja mmoja ambako watu wengine wanaendelea kuzuiliwa.
Amesema walipofika kwenye uwanja huo waliamriwa kulala chini huku maafisa hao, wakiwafanyia uchunguzi mmoja baada ya mwingine.
chanzo bbc.com

No comments:

Post a Comment