Wednesday, November 7, 2012

Watanzania wanena juu ya Ushindi wa Baraka Obama huko Marekani.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu, amesema kuwa Tanzania inapaswa kujifunza kutoka kwenye uchaguzi uliofanyika nchini Marekani juzi, ili kuepuka matumizi makubwa ya fedha ndani ya vyama.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Profesa Baregu, alisema kuwa uchaguzi wa Marekani umemalizika huku kukiwa na matumizi makubwa ya fedha kwa vyama hivyo viwili, hivyo Tanzania inapaswa kujiepusha na mfumo huo.
Baregu ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya, alifafanua kuwa hapa nchini kumekuwa na matatizo ya matumizi ya fedha hatua inayowafanya baadhi ya Watanzania kuogopa kuwania uongozi.
Alisema kuwa, iwapo tatizo hilo halitadhibitiwa ndani ya vyama, kuna uwezekano mkubwa kwa watakaowania uongozi kuwa ni watu walio na uwezo wa kifedha.
Msomi huyo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, aliongeza kuwa iwapo kutakuwa na udhibiti wa matumizi ya fedha katika chaguzi mbalimbali, kundi kubwa litaweza kugombea uongozi na hivyo demokrasia kuzidi kukua.
“Kama kutakuwepo na matumizi makubwa ya fedha hata watakaogombea itaonyesha kuwa hawachaguliwi, bali wananunua uongozi,” alisema.
Naye, Mchungaji William Mwamalanga alisema kuwa, jambo kubwa la kujifunza kwa Marekani ni kwa wanasiasa wa Tanzania kuwa tayari kukubali matokeo pale wanaposhindwa ili kujiepusha na matumizi ya rushwa katika chaguzi.
Alisema kuwa taifa la Marekani limepiga hatua kutokana na kujiepusha na matumizi ya rushwa kwani wagombea wote hujinadi kwa sera zao kuliko ilivyo kwa hapa nchini.
Mwamalanga alisema hatua ya kuendelea kuikumbatia rushwa, watu kushindwa kujitokeza katika kuchagua viongozi, ndiyo sababu ya idadi ya wapigakura kuzidi kushuka mwaka hadi mwaka.
“Tumeona wenzetu walivyoweka utaifa mbele kuliko vyama, watu wanaenda kusikiliza kampeni na kuhoji sera na wala hakuna vibendera maana wanautanguliza utaifa mbele,” alisema.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi nchini (Tucta), Nicholaus Mgaya, aliupongeza uchaguzi wa Marekani uliomwezesha Rais Obama kurejea madarakani, na kuitaka Tanzania kuiga mfano huo.
Akizungumza na Tanzania Daima kuhusu uchaguzi huo, alisema demokrasia imechukua mkondo wake kwani kushinda ni mambo ya kawaida, kusionekane chama fulani ndicho chenye kushinda wakati wote hata kama hakifai.
Alitoa rai kwa serikali kutokuwa na mawazo kwamba wakati wa uchaguzi chama kingine kikiingia madarakani kitaharibu nchi.
Mgaya alisema uchaguzi wa Marekani uwe funzo kwa wapigakura nchini kufuata nyayo zao kwa kuwa na uwezo wa kuamua kumchagua kiongozi wanayemtaka kulingana na uwezo wake.
Mwananchi mwingine, Abdullah Saiwaad, alisifu demokrasia iliyotumika wakati wa uchaguzi huo hasa kuheshimiana kati ya wagombea.
Saiwaad ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Readit Books, alimsifu hasimu wa Obama, Romney kutokana na kukubali matokeo alipoona anaelekea kushindwa.
Pia alisifu hotuba ya Obama kukubali kushirikiana na watu wa Republican kutafuta umoja.
“Uchaguzi huo ni mfano wa kuigwa kwa sababu tunatofautiana katika kuchagua, lakini lazima anayeshindwa atoe ushirikiano kwa aliyeshinda ili kujenga Tanzania yenye maendeleo,” alisema.

No comments:

Post a Comment