Saturday, November 3, 2012

Swali la Zitto lamchanganya Waziri Mambo ya ndani

SERIKALI jana ilishindwa kujibu swali bungeni juu ya mlo kamili kwa wafungwa na mahabusu lililoulizwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema).
Hata hivyo, kulitokea mgongano katika jibu la swali hilo kwani Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya ndani, Pereila Silima awali alishasema wanakula mara tatu jambo lililoonyesha kupingwa na Waziri wake Dk, Emanuel Nchimbi.
Katika swali lake la nyongeza lililoelekezwa kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Zitto alitaka kauli ya Serikali kama wafungwa na mahabusu wanapata chakula mara ngapi kwa siku.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk Nchimbi, alijibu kwa mkato swali hilo na kusema “Taratibu za kazi hazitamkwi bungeni hivyo kuna mamlaka kamili na maeneo ambayo yanaweza kuzungumziwa.”
Katika swali la msingi, Jaku Hashim Ayub (Baraza la Wawakilishi-CCM) alitaka kujua Serikali inatenga kiasi gani kwa mwaka kwa ajili ya huduma za chakula kwa mahabusu na vituo vya polisi Zanzibar.
Mbunge huyo alihoji pia iwapo Serikali itakuwa na taarifa kuwa askari kulazimika kukopa au kutumia fedha zao kuwanunulia mahabusu chakula na huduma nyingine licha ya kuwa mishahara yao ni midogo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereila Ame Silima alisema kuwa kiasi cha fedha kinachotengwa kwa ajili ya kulisha mahabusu kwa nchi nzima hutofautiana mwaka hadi mwaka kutegemea na ukomo wa bajeti ya wizara.
“Kwa mfano, mwaka wa fedha 2009/10 vituo vya polisi Zanzibar vilitengewa Sh130 milioni na mwaka 2010/11 Sh100 milioni zilitengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Kuhusu taarifa za askari kununua chakula kwa ajili ya wafungwa na mahabusu kwa kutumia fedha zao, alisema Serikali haina taarifa hizo hadi sasa kwani jukumu hilo ni la Serikali wakati wote.

No comments:

Post a Comment