RAIS Jakaya Kikwete ameikataa ramani ya awali ya Jiji la Arusha
iliyowasilishwa ofisini kwake, baada ya kugundua kuwa haiko kiuhalisia
baada ya kujumuisha maeneo ya vijiji vyenye shughuli ya kilimo na
ufugaji visivyoruhusiwa ndani ya Jiji.
Akihutubia mkutano wake wa
kwanza wa hadhara mjini Arusha tangu mwaka 2010, mara baada ya kuzindua
Jiji la Arusha juzi, Rais Kikwete aliuagiza uongozi wa Jiji na serikali
mkoani Arusha kuandaa ramani mpya itakayozingatia na kukidhi mahitaji
na uhalisia kwa kuondoa maeneo ya vijiji.
Aliuambia umati wa
wananchi waliohudhuria mkutano uliofanyika uwanja Sheikh Amri Abeid kuwa
ramani ya awali aliyoikataa inataja Manispaa tatu zitakazounda Jiji la
Arusha kuwa ni Arumeru Mashariki,Arumeru Magharibi na Arusha Mjini.
ìKwa
tafsiri hiyo ina maana maeneo ya vijiji kama Ngarenanyuki,Oldonyo Sambu
na sehemu zingine ambazo shughuli kuu ya wananchi ni kilimo na ufugaji
ambayo kisheria hayaruhusiwi ndani ya Jiji yatakuwa sehemu ya Jiji la
Arusha,î alisema Rais Kikwete
Wakazi wengi wa wilaya ya Arumeru
inayoundwa na Halmashauri za Meru (Arumeru Mashariki) na Arusha DC
(Arumeru Magharibi) ni wafugaji kutoka makabila ya Kimaasai, Kiarusha na
Kimeru ambao njia yao kuu ya uchumi ni ufugaji wa kuchunga na kilimo.
Iwapo, Rais angekubaliana na ramani iliyowasilishwa kwake, shughuli
zote
za ufugaji na kilimo zingepigwa marufuku na hivyo kuathiri maisha ya
wananchi wengi wa wilaya ya Arumeru, ambao wangelazimika kutafuta njia
nyingine ya kumudu maisha yao, jambo ambalo lingeibua mgogoro wa
kimaslahi kati yao na serikali.
Kabla ya kupanda hadhi kuwa Jiji,
eneo la Halmashauri ya Manispaa ya Arusha ilikuwa ni Kilomita za Mraba
93. Eneo hilo limeongezeka hadi kufikia Kilomita za Mraba 208 baada ya
baadhi ya sehemu na Kata za wilaya ya Arumeru kumegwa na kuhamishiwa
wilaya ya Arusha.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ujenzi, Dk
Jahn Magufuli, ameuagiza uongozi wa Jiji la Arusha kuhakikisha ujenzi wa
barabara kwa kiwango cha lami unaoendelea Jijini humo unazingatia
mahitaji na kukua kwa mji kwa zaidi ya miaka 50 ijayo.
ìBarabara
za Jiji zinatakiwa kuwa za njia tatu, nne na hata nane kwa kutilia
maanani mahitaji na kukua kwa miji. Tusijenge barabara za kubanabana
kama vile Jiji letu halitakua,î alisema Dk Magufuli.
Barabara
kadhaa zenye urefu wa zaidi ya kilomita 14 za Jiji la Arusha ziko kwenye
ujenzi kwa kiwango cha lami ikiwa ni mpango wa maboresho ya miji nchini
unadhaminiwa na mikopo kutoka Benki ya Dunia (WB), taasisi na wadau wa
maendeleo.
Wakati Dk Magufuli akitaka ujenzi wa barabara za Jiji
kuzingatia mahitaji ya miaka 50 ijayo, Jiji la Arusha linakabiliwa na
changamoto ya kutoweza kupanua barabara zake za katikati ya Jiji hata
kufikia njia mbili kutokana na barabara zote kuu kuzingirwa na maghorofa
ambayo gharama ya kuzibomoa zinaweza kutoka kuanzisha mji mwngine mpya.
No comments:
Post a Comment