Monday, November 5, 2012

Rais Kikwete atekeleza ahadi Himo,JIBU LA SWALI LA MBUNGE Vunjo

AHADI ya Rais Jakaya Kikwete ya kupeleka fedha katika mji wa Himo kwa ajili ya kusaidia mradi wa maji, imetekelezwa.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Kassim Majaliwa, na kuongeza kuwa ahadi hiyo imetekelezwa kwa awamu mbili.
Naibu Waziri alisema ahadi ya Rais ilitekelezwa kwa kupeleka sh milioni 50 Februari mwaka huu kabla ya kumaliza ahadi yake kwa kupeleka sh milioni 100 ambazo zilitumwa Julai mwaka huu.
Alisema fedha hizo zilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Moshi, ili zitumike kukamilisha utekelezaji wa mradi wa maji kutoka chanzo cha Mananga.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri, upatikanaji wa maji katika mji wa Himo kwa sasa ni wa kuridhisha ambapo wakazi wake wanapata maji safi na salama kwa saa 24 kila siku.
Naibu Waziri huyo alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema (TLP), aliyetaka kujua ni lini serikali itatekeleza ahadi iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete katika kipindi cha kampeni kuwa atapeleka fedha kwa ajili ya mradi wa maji katika mji wa Himo.
Pia alihoji ni lini tatizo la maji litamalizika katika mji wa Himo ambao unakua kwa kasi na kuwa na mahitaji ya maji.

No comments:

Post a Comment