Monday, November 5, 2012

Abeidi Pele kupeleka Serengeti Boys Ulaya

Nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ghana na Olympique Marseille ya Ufaransa, Abeidi Pele ameahidi kuwapeleka katika klabu kubwa za Ulaya na kwingineko duniani yosso wote watakaofanya vizuri katika timu ya taifa ya vijana (Serengeti Boys) na wachezaji wengine wenye vipaji vya soka nchini.

Pele aliyasema hayo wakati akizungumza na wachezaji wa Serengeti Boys kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam jana.

Pele, ambaye alikuwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) alisema kuwa Tanzania ina vijana wengi wenye vipaji vya soka lakini hawachezi katika klabu zinazoshiriki ligi maarufu duniani kwa vile hawajafikiwa vya kutosha na wasaka vipaji wa kimataifa.

"Tanzania ina wachezaji wengi nyota, mimi na rais Leodegar Tenga tutashirikiana kuhakisha wasaka vipaji wengi wanafika Tanzania ili kuwachukua vijana wazuri na wenye vipaji," alisema Pele.

"Waafrika wengi wanaong'ara na klabu za Ulaya wanatoka Ghana, Ivory Coast, Nigeria... kwanini wasiwe Watanzania? Nafikiri kuna haja sasa ya kuleta wasaka vipaji wengi zaidi. Huu ndiyo msaada pekee ninaoweza kuutoa kwenu,” alisema.

"Lazima muwe na bidii, nidhamu na mfanye kazi kwa kujituma. Wachezaji nyota mnaowaona duniani wamefanikiwa kwa sababu wanafanya kazi kwa bidii na wanajituma sana, hasa katika kufanya mazoezi."

Pele ambaye hivi sasa ni mmoja wa maafisa wa Kamati ya Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na FIFA, alisema Tanzania inaweza kufuzu kwa mara nyingine katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kama ilivyofanya mwaka 1980 endapo wachezaji, hasa vijana watacheza kwa kujituma na kufuata maelekezo ya makocha.

Alisema hata wanaye, Abdulrahim, Ayew na Jordan wamepata mafanikio kisoka kwa sababu wanafanya mazoezi kwa bidii. Abdulrahim yuko katika klabu ya Lierse SK ya Ubelgiji wakati Ayew na Jordan wako katika klabu ya zamani ya baba yao ya Olympique Marseille inayoshiriki Ligue 1, Ligi Kuu ya Ufaransa.

"Hakuna njia ya mkato katika kupata mafanikio kwenye mchezo wa soka. Nidhamu, bidii na kutekeleza ipasavyo maelekezo ya wataalam wa ufundi ndizo nguzo muhimu katika kufanikiwa," alisema nyota huyo ambaye leo anasherehekea miaka 48 tangu alipozaliwa Novemba 5, 1964.

"Kipaji hakitoshi kwa soka la sasa, Lazima tuweke nguvu katika mazoezi. Wale wasio na vipaji wakifanya mazoezi kwa nguvu nao wanakuwa sehemu ya mafanikio ya timu," aliongeza Abedi Pele.

Naye Afisa Maendeleo wa FIFA, Ashford Mamelodi aliwataka vijana kucheza kwa bidii ili kuipa heshima Tanzania, kama ilivyokuwa mwaka 1980.

Nahodha wa Serengeti Boys, Hussein Abdallah alimshukuru Abedi Pele na viongozi wa FIFA kwa kutembelea Tanzania na kuwapa wachezaji vijana moyo wa kujituma, hasa wa timu yake.


CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment