Saturday, November 3, 2012

Hatma Simba, Yanga kileleni mikononi mwa Azam, Mtibwa

LIGI Kuu ya soka Tanzania Bara, inaendelea kutimua vumbi leo ambako matokeo ya Morogoro na Dar es Salaam yanatarajiwa kubadilisha msimamo wake ambao hadi sasa Simba inaongoza kwa tofauti ya wastani wa bao moja.
Simba, mabingwa watetezi wako kileleni wakiwa na pointi 23 sawa na watani zao Yanga wenye pointi kama hizo, lakini wakizidiwa kwa tofauti ya wastani wa bao moja, ambako timu zote zimeshuka dimbani mara 11 huku nafasi ya tatu ikikamatwa na Azam FC wenye pointi 21 iliyocheza mechi 10.
Kwenye dimba la Jamhuri Morogoro, Simba watakuwa na kibarua kizito dhidi ya Mtibwa Sugar, huku dimba la Taifa jijini Dar es Salaam, shughuli itakuwa pevu kati ya Yanga na Azam FC.
Matokeo ya mechi hizo, yanatarajiwa kubadilisha msimamo wa ligi hasa kwa nafasi za juu, ambako huenda baadhi ya timu zikapata ahueni au maumivu zaidi.
Endapo vinara Simba waliojichimbia huko Moro na Yanga walioko Bagamoyo, wakipoteza, basi Wana lambalamba ambao wamemrejesha kwa kishindo kocha wao waliyemtupia virago awali, Stewart Hall, watakamata usukani wa ligi na kuviacha vigogo hivyo vikiumana katika nafasi ya pili na tatu.
Lakini vile vile, Simba au Yanga wakishinda, mmojawapo atakuwa kileleni kulingana na idadi na mabao watakayokuwa wamevuna.
Mechi kati ya Yanga na Azam inatarajiwa kuwa ngumu na yenye upinzani mkubwa, hasa ukizingatia viwango vya timu zote mbili.
Azam imetoka kuisulubu Coastal Union kwa mabao 4-1 ikiwa chini ya Hall, huku Yanga ikishinda 3-0 dhidi ya Mgambo JKT, hivyo mechi ya leo inatarajiwa kuwa na ushindani na mvuto wa aina yake, achilia mbali matokeo ambayo yana faida kubwa kwa kila timu.
Mjini Morogoro, Simba ambayo inaandamwa na sare katika mechi za ugenini, inatarajiwa kukumbana na upinzani mkali kutoka kwa Wakata Miwa hao wa Manungu Turiani, ambao wana rekodi ya kuwakalisha vigogo wengine Yanga kwa mabao 3-0. Mtibwa imetoka kuilaza JKT Oljoro kwa mabao 2-1 jijini Arusha.
Hivyo kwa leo, unaweza kusema Azam na Mtibwa zimeshikilia hatima za Simba na Yanga katika mchuano wa kuongoza ligi hiyo ambayo imebakiza takribani mechi mbili kumaliza mzunguko wa kwanza.
Je, nani kilio, nani kicheko leo? Ni jambo kusubiri na kuona.

No comments:

Post a Comment