Thursday, November 8, 2012

Wagoni wazua tafrani Dar,ni waliogandana huko Temeke

Polisi wakiwa tayari kuwadhibiti wananchi wakiofurika katika Hospitali ya Temeke jana ili kushuhudia watu wawili waliodaiwa kupelwekwa hospitali wakiwa wamenasana katika tendo la ndoa

HEKAHEKA ya aina yake, ilitokea jana kwenye Hospitali ya Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, baada ya kudaiwa kuwapo na watu waliokuwa wamefanya uzinzi na kushindwa kutengana.
Tukio hilo lililozusha sintofahamu, lilidaiwa kutokea kwenye nyumba moja ya kulala wageni (jina tunalo) iliyopo Temeke na wahusika walipoona wanashindwa kujinasua baada ya kumaliza haja zao, waliomba msaada wa kufikishwa hospitalini hapo.
Habari hizo zilizoanza kuenea majira ya asubuhi zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii na mikoa mbalimbali jambo lililosababisha baadhi ya wasomaji kupiga simu katika chumba cha habari kutaka kujua nini hasa kilichotokea.
Mashuhuda wa tukio hilo, waliliambia Mwananchi kuwa watu hao walifikishwa hospitalini hapo wakiwa kwenye gari aina ya Canter kwa ajili ya kupatiwa huduma baada ya kila mmoja kumng'ang'ania mwenzake huku wakiwa wamejifunika shuka za nyumba hiyo ya kulala wageni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime alipofuatwa kuzungumzia tukio hilo lililotokea mita takriban 300 kutoka ofisini kwake, ilielezwa kuwa yuko kwenye kikao.
Hata hivyo, alipotafutwa baadaye jioni alisema: “Habari hizo ni uongo, hazina ukweli wowote, na polisi imeanza uchunguzi kufahamu nani aliyeanzisha uvumi huo.”
Kwa mujibu wa Kamanda Misiime, ambaye anahamia Dodoma kuchukua nafasi ya Kamanda Zelothe Steven anayestaafu, alisema polisi wanaendelea na doria hadi hapo hali itakapotengemaa katika hospitali hiyo.

Kinachodaiwa kutokea Hospitali ya Temeke
"Muda wa saa 4:00 asubuhi liliingia gari aina ya Canter hospitalini huku likiwa na watu wawili ambao walifunikwa shuka na kupelekwa katika ofisi zilizopo kwenye jengo la kuhifadhiwa maiti," alisema mmoja wa mashuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Khamis Ramadhani.
Alisema: "Habari hizi zilienea kwa kasi na kuvuta hisia za wengi na walifika hospitalini hapo kwa ajili ya kuwashuhudia watu hao.
"Baada ya kutokea hali hiyo, Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU)  walifika kwa ajili ya kuwatawanya baada ya kuanza ghasia huku wengine wakitumia nafasi hiyo kupora mali kwa watu wengine."
Mwandishi wa habari hizi, alishuhudia Polisi ikiwatangazia watu kuondoka eneo hilo vinginevyo watatumia nguvu.
Baada ya watu kutotii amri ya kuondoka, polisi hao walianza kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya watu hao.
Hata hivyo, watu hao waliondoka eneo la tukio, lakini baadaye walirudi tena na askari  kulazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Baada ya kuona hali inazidi kuwa ngumu, uongozi wa  hospitali hiyo ulifunga milango na kuzuia watu kuingia ndani wakiwamo wagonjwa wa nje waliofika kwa ajili ya kutibiwa.

No comments:

Post a Comment