Wednesday, November 14, 2012

Tundu Lissu: Madaraka ya Rais yapunguzwe

MBUNGE wa Jimbo la Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu amesema kuwa katika Katiba Mpya kunatakiwa kuwa na kipengele cha kumpunguzia Rais madaraka, ikiwa ni pamoja na kulivunja Bunge.


Katiba ya sasa Ibara ya 90 (2) inaeleza kuwa Rais atakuwa na uwezo wa kulivunja Bunge kama limemaliza muda wa uhai wake, kama limekataa kupitisha bajeti iliyopendekezwa na Serikali.

Pia anaweza kulivunja kama litakataa kupitisha muswada wa sheria, kama limekataa kupitisha hoja ambayo ni ya msingi katika sera za Serikali.

Lissu ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni aliyasema hayo wakati akitoa maoni yake juu ya Katiba Mpya katika Kata ya Ikungi wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Katika mkutano huo wa utoaji maoni, Lissu ndiye aliyekuwa mtu wa mwisho kutoa maoni yake, ikiwa ni baada ya zaidi ya wananchi 25 wa Kata hiyo kutoa maoni yao.

Katika maelezo yake anasema Katiba Mpya inatakiwa kupunguza madaraka ya Rais ikiwa ni pamoja na kuwa na kipengele kitakachoeleza kuwa Rais sio sehemu ya Bunge, hivyo kukosa nguvu ya kulivunja Bunge.

Anasema kuwa sheria hiyo itaweza kutenganisha uchaguzi wa wabunge na rais, anapendekeza kwamba uchaguzi wa rais ufanyike miaka miwili baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa wabunge, lengo likiwa ni kulifanya Bunge kuwa la kudumu.
Anasisitiza kwamba Bunge na Serikali inatakiwa kujiendesha bila kuingiliana na anasisitiza; “Bunge linatakiwa kuwa la wabunge sio Rais.”

Anasema kuwa Katiba Mpya inatakiwa kueleza wazi kwamba Rais sio sehemu ya Bunge na asiwe na uwezo wa kuteua wabunge kama ilivyo sasa.
Anasema kuwa Rais abaki na mamlaka ya kuteua mawaziri, lakini mawaziri hao iwe lazima kuthibitishwa na Bunge.

“Mbali na kumuondolea uwezo wa kuteua wabunge katika zile nafasi 10 za uteuzi wake, pia Rais asiteue Katibu wa Bunge, Katibu ateuliwe na tume ya utumishi wa Bunge,” anasema Lissu na anaongeza;
“Majaji nao wanatakiwa kutoteuliwa na Rais bali wapatikane kupitia ndani ya mahakama.”
Anazungumzia wingi wa wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Lissu anasema kuwa Katiba Mpya inatakiwa kutamka idadi kamili ya wabunge.

“Nataka ukubwa wa bunge uthibitishwe na Katiba Mpya, ieleze kwamba idadi ya wabunge ni kiasi fulani” anasema Lissu na anaongeza;

“Siwezi kusema idadi ya kamili ya wabunge kwa kuwa suala hilo linahitaji mjadala mpana ila binafsi nataka idadi ya wabunge iwe hiyo hiyo kila unapofanyika uchaguzi.”
Anafafanua kuwa nafasi za ubunge wa Viti Maalum zisiwepo, badala yake yawepo majimbo maamlum kwa ajili ya kugombewa na wanawake.

“Wabunge wanawake wachaguliwe na wananchi moja kwa moja, najua kuwa bungeni wapo asilimia 30, napendekeza ibaki hiyohiyo ila watengewe majimbo yao maalum ambayo watakuwa wakijinadi na kupigiwa kura na wananchi,” anasema Lissu.
Anasema kuwa ndani ya Katiba Mpya kunatakiwa kuwe na mfumo wa Serikali Kuu na Serikali za mikoa.

“Kuwe na utaratibu wa wananchi kuchagua viongozi ngazi ya mkoa ili viongozi hao wawajibike moja kwa moja kwa wananchi,” anasema.
chanzo-gazeti la mwananchi

No comments:

Post a Comment