BARAZA la Madiwani wa Halmashauri Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara,
limeridhia asilimia 50 ya hisa za Kampuni ya TanzaniteOne zigawanywe
kabla ya kampuni hiyo kupewa upya leseni ya uchimbaji madini.
Akisoma
azimio hilo kwenye Baraza la hilo juzi, Makamu mwenyekiti wa
halmashauri hiyo, Jackson Sipitek alisema wadau wengine wanatakiwa
kupata hisa ya asilimia 50 kama sheria mpya ya madini ya mwaka 2010
inavyoelekeza.
Sipitek alisema Kampuni ya TanzaniteOne itabakiwa na
asilimia 50 ya hisa, zilizosalia zitagawanywa kwa halmashauri ya wilaya
hiyo na nyingine zitauzwa kwa wananchi kupitia soko la hisa.
Alisema
hisa nyingine zilizobakia zitauzwa kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo na
nyingine kwenye Wizara ya Nishati na Madini kupitia Shirika la Madini la
Taifa (Stamico).
Alisema Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya
Halmashauri ya Wilaya na baraza hilo waliwateua viongozi wanne kukutana
na Wizara ya Nishati na Madini, TanzaniteOne na wadau wengine kujadili
jambo hilo.
Aliwataja viongozi hao kuwa, ni Mbunge wa jimbo hilo,
Christopher Ole Sendeka, Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Peter
Tendee, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri, Muhammed Nkya na Mweka
hazina wa wilaya, Peter Mollel.
Hali hiyo inahitimisha sintofahamu ya
muda mrefu baina ya wachimbaji wadogo na serikali, baada ya wachimbaji
hao kudai kutokana na leseni ya kampuni hiyo kumaliza muda wake Agosti
mwaka huu, watapatiwa eneo hilo.
Wachimbaji hao wadogo walidai kuwa,
walitarajia serikali itasikia kilio chao cha muda mrefu cha kuwapatia
eneo hilo, kwani madini ya vito hasa Tanzanite hayapaswi kuchimbwa na
wageni.
Walisema Rais Jakaya Kikwete mwaka 2010 alipokuwa anaomba
kura mjini Orkesumet, wilayani Simanjiro aliwaahidi baada ya leseni ya
kampuni hiyo kumaliza muda wake atawapa eneo hilo, ahadi ambayo
hajaitekeleza.
Hata hivyo, sheria mpya ya madini ya mwaka 2010 ambayo
ilipitishwa na Bunge baada ya mapendekezo ya Tume ya Jaji Mark Bomani
ya mwaka 2008, inaeleza madini hayo yakichimbwa na wageni wamiliki
asilimia 50 ya hisa na wazawa 50.
No comments:
Post a Comment