Monday, November 5, 2012

Simba kwawaka moto • Kaburu, Kaseja wapewa siku mbili

BAADA ya kichapo cha mabao 2-0 kutoka Mtibwa Sugar juzi, wanachama na mashabiki wa Simba jana walivamia makao makuu ya klabu yao, Msimbazi Kariakoo, jijini Dar es Salaam, wakiwa na mabango yakimtaka Makamu Mwenyekiti Geofrey Nyange ‘Kaburu’ na nahodha Juma Kaseja kubwaga manyanga.
Mashabiki na wanachama hao, ambao walifurika klabuni hapo kuanzia majira ya saa 4 asubuhi, huku wakiimba nyimbo mbalimbali za kumtaka Kaseja na Kaburu kuwaachia Simba yao ndani ya siku mbili, kutokana na mwenendo mbaya wa timu yao.
Akizungumza kwa hasira, mmoja wa wanachama wa timu hiyo, Saidi Msako mwenye kadi namba 1110, alisema wameamua kufikia hatua hiyo, kutokana na uongozi wao kufanya ubabaishaji, hususan katika mchezo wa juzi, ambapo Kaburu alimwamuru Kocha Mkuu, Milovan Cirkovic, kupanga wachezaji ambao anawataka yeye.
Msako alisema yeye binafsi alikwenda Morogoro ambako awali Milovan alimpanga Masoud Cholo, Ngasa na Hassan Hatibu katika kikosi cha kwanza, huku Kaseja akiwa hayumo, lakini Kaburu alishinikiza kuwaanzisha Paschal Ochieng, Komambil Keita na Daniel Akuffor ambao wote hawana uwezo.
Naye Mgeni Ramadhan ‘Macho’ mwenye kadi namba 2426, alitupa lawama kwa uongozi huo, huku akisema Kaburu anawaweka wachezaji katika matabaka na juu ya hilo, wamemvumilia wamechoka, huku akimpongeza Mwenyekiti wa Kamati ya usajili Zacharia Hanspope kwa kuwa na moyo na kujaribu kuwaweka wachezaji katika hali sawa.
“Tunamshangaa Kaburu anang’ang’ania nini, kama sio maslahi ndani ya Simba yetu, maana kila kitu ni yeye, suala la Kelvin Yondani kwenda Yanga yeye, Ulimboka Mwakingwe yeye, Emmanuel Okwi kutaka kwenda Yanga yeye, sasa basi tumemchoka na tunampa siku mbili yeye na Kaseja,” alisema Macho.
Wanachama hao waliendeleza zogo klabuni hapo hadi majira ya saa 9 mchana, huku Gosbert Peter ambaye alijiita shabiki wa kulia, akisema ni bora icheze timu ya watoto ‘Simba B’ ambayo inafanya vema kuzidi hao waliokula chumvi nyingi bila ya kuwa na umuhimu wowote.
Wanachama hao walionekana kukerwa na uongozi wao, ambao ulimpa Milovan mechi tatu kwa lengo la kumtimua, ambapo walibeba mabango kadhaa yaliyokuwa na maneno ‘Kocha wetu Milovan bado tunakuhitaji mchango wako mkubwa’, ‘Kaburu hatukutaki, Kaseja tuachie Simba yetu’, ‘Wachezaji mamluki mjirekebishe, Simba mmeikuta’, ‘Ndugu Kaburu pamoja na Kaseja, Simba yetu tumewachoka’.
Wakati wanachama hao na mashabiki wakiondoka, alijitokeza mwanachama mwenye kadi namba 00711 Salum Seleman ‘Kada’ ambaye aliutaka uongozi kuheshimu na kufuata katiba ya klabu yao inavyosema, ikiwa ni pamoja na kuitisha mkutano mkuu ambao mpaka sasa unafanywa kinyemela kwa maslahi ya watu.
Simba kwa sasa inashika nafasi ya pili, ikiwa na pointi 23 huku Yanga ambayo ilianza kwa kuchechemea ikishika usukani kwa pointi 26 huku Azam ikikamata nafasi ya tatu kwa point 21.

No comments:

Post a Comment