KATIBU wa Bunge Dk. Thomas Kashililah, amesema kuwa taarifa kuhusu
ripoti ya kamati ndogo iliyoundwa kuchunguza tuhuma za wabunge
kujihusisha na vitendo vya rushwa, itawasilishwa bungeni siku yoyote
kuanzia leo katika mkutano unaoendelea sasa.
Dk. Kashililah aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na gazeti hili,
akitakiwa kufafanua kuhusiana na ripoti hiyo na kile kinachoaminika
kuwa ni msimamo wa Spika Anne Makinda, kutotaka ripoti hiyo isisomwe
bungeni.
“Kwa mujibu wa Sheria ya 296 inayohusu Haki, Kinga na Madaraka ya
Bunge hili jambo linahusu haki, ni lazima taarifa yake itawasilishwa,”
alisisitiza Dk. Kashililah.
Hata hivyo, licha ya kulihakikishia gazeti hili kuwa ripoti hiyo
itawasilishwa bungeni lakini alikataa kutaja ni siku husika na
kusisitiza kuwa tayari Spika amekwishaifanyia kazi.
Dk. Kashililah alisema Spika hajaing’ang’ania ripoti hiyo kama ambavyo
wengi wamekuwa wakiamini na kwamba uamuzi wowote utakaofanywa kuhusu
ripoti hiyo utakuwa ni wa wazi.
Alisema baada ya Spika kuifanyia kazi ripoti hiyo, ataamua kama yeye
aiwasilishe au airudishe kwenye kamati hiyo iliyokuwa ikiongozwa na
Brigedia Hassan Ngwilizi, itoe taarifa.
Kuhusu taarifa ya ripoti hiyo kutokuwamo kwenye ratiba za shughuli za
Bunge, Dk. Kashililah alisema hilo halimzuii Spika kupanga utaratibu
wake wa kuipeleka bungeni.
“Spika anapotaka kuliingiza jambo kwenye shughuli za Bunge hahitaji
kuliweka katika ratiba, atakapoamua itaingizwa kwenye Order Paper
(ratiba inayoonyesha shughuli za Bunge kwa siku)…mamlaka anayo, anaweza
kurekebisha,” alisema.
Kwa mujibu wa ratiba ya mkutano wa tisa wa Bunge, leo baada ya kipindi
cha maswali na majibu, utawasilishwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria
mbalimbali ya mwaka 2012.
Kesho baada ya kipindi cha maswali, kutakuwa na tathmini ya matumizi
ya Kanuni za Kudumu za Bunge siku ambayo pia huenda suala la taarifa ya
ripoti hiyo ya Ngwilizi ikaingizwa kwenye ratiba.
Alhamisi ratiba inaonyesha kuwa kutakuwa na maswali kwa Waziri Mkuu na
baada ya hapo, yatafuata maswali ya kawaida kisha hoja binafsi za
wabunge na Ijumaa baada ya maswali kutakuwa na hoja binafsi za wabunge
kabla ya kuahirisha Bunge.
Tangu kamati ya Ngwilizi imalize uchunguzi wake na kukabidhi ripoti
kwa Spika, kumekuwepo na taarifa kadhaa zikidai kuwa Makinda anakataa
ripoti hiyo isijadiliwe kwa maelezo kuwa anahitaji muda kuifanyia kazi.
Makinda alitoa uamuzi wakati wa kikao cha wabunge wote kilichokuwa kikijadili ratiba ya shughuli za Bunge hili la tisa.
Bila kutoa ufafanuzi wa kina, Spika Makinda alisema yeye ndiye anajua
lini na wakati gani wa kuileta hoja hiyo bungeni na kamwe hawezi kuileta
kwa shinikizo la wabunge.
Hata hivyo, hatua hiyo iliibua maswali kutoka kwa baadhi ya wabunge
waliotaka kujua sababu za kutoileta ripoti hiyo ijadiliwe bungeni,
lakini Spika hakutaka kutoa ufafanuzi na badala yake alisisitiza kwamba
haitajadiliwa katika mkutano huo wa Bunge.
Makinda anaelezwa kuwa asingeweza kuileta ripoti hiyo bungeni kwani
uchunguzi umebaini hakuna mbunge aliyejihusisha na rushwa wakati tayari
alishavunja Kamati ya Nishati na Madini kwa tuhuma hizo.
Wajumbe wengine waliomo kwenye kamati ya Ngwilizi ambaye pia ni mbunge
wa Mlalo ni Saidi Arfi (Mpanda Kati), John Chiligati (Manyoni
Mashariki), Goesbert Blandes (Karagwe) na Riziki Omary Juma (Viti
Maalumu).
chanzo-Tanzania daima

No comments:
Post a Comment