Monday, November 5, 2012

PELE IN TANZANIA TOUR,AVUTIWA NA VIPAJI VYA TANZANIA.

BALOZI wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Abeid Ayew ‘Pele’ ameelezea kukunwa na vipaji lukuki vilivyopo hapa nchini huku akilipongeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kuthubutu na kuendeleza timu za vijana kwa mujibu wa FIFA.
Pele nyota wa zamani wa Ghana, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Maalum ya FIFA, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, alipozungumza na waandishi wa habari, baada ya kuiona timu ya vijana ya Serengeti Boys, pamoja na mchezo wa juzi kati ya Azam na Yanga.
“Tanzania ni moja ya nchi ambazo zimebarikiwa vipaji na hii nimeona mwenyewe kwa macho yangu, licha ya kuwa ni mara ya kwanza kuja hapa nchini ila nimefarijika sana, kuna vipaji, cha muhimu ni kuviendeleza zaidi, maana mchezo wa jana kati ya Yanga na Azam ni mchezo ambao ulinivutia sana,” alisema Pele.
Aidha alisema amekuja Tanzania kwa lengo la kuangalia miradi, sambamba na kutathmini kuanzia kwa watoto wadogo hadi Copa Coca-Cola, ili kukuza mchezo huo na kupata wachezaji ambao watafanya vema ndani na nje ya nchi.
Alisema ataendelea kuja hapa nchini kutokana na vipaji ambavyo ameviona, vinavyoweza kuzaa matunda mazuri hapo baadaye.
Pele aliongeza kuwa mpira unakuzwa na wanahabari ambao wanaweza kuufanya kushuka au kupanda, ambapo wanatarajia kuanzisha semina kwa wanahabari mwanzoni mwa mwaka ujao, ili kuzidi kuwaongezea ujuzi zaidi na mpira uzidi kukua.
Naye Mwenyekiti wa Maendeleo ya Soka Kanda ya Afrika, Ashford Mamelodi, ambaye aliambatana na Pele, alisema, wana mpango mkubwa wa kuendeleza soka hapa nchini, ikiwa ni pamoja na kuufanyia marekebisho uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza na baadaye Zanzibar.
“Tuna mpango endelevu kama ambavyo tulifanya uwanja wa Karume na Uhuru, Nyamagana Mwanza tuna mpango wa kufanya hivyo na tunazidi kuipenda Tanzania kutokana na vipaji ambavyo tunaviona,” alisema Mamelodi.

No comments:

Post a Comment