MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (Chadema), amethibitisha kuwa anaumwa na anapatiwa matibabu nchini Uingereza.
Hata
hivyo, amesema hadi jana alikuwa anaendelea vizuri na anasubiri uamuzi
wa daktari wake kumruhusu atoke hospitalini. Ndesamburo alitoa kauli
hiyo alipokuwa anazungumza na gazeti hili juzi usiku.
“Ni kweli
naumwa, lakini sijazidiwa hata kidogo si hata wewe (mwandishi) si
unanisikia ninaongea na wewe vizuri kabisa ningekuwa nimezidiwa
tusingeongea hivi,” alisema Ndesamburo.
Mbunge huyo amewatoa hofu
wananchi wa Jimbo lake kuwa afya yake ni imara baada ya kupatiwa
matibabu na mara madaktari wake watakapomruhusu atarejea nchini.
Hata
hivyo, Ndesamburo hakuweka wazi ugonjwa unaomsumbua, lakini akisisitiza
kuwa suala la kuumwa kwa binadamu ni la kawaida na kwamba hali yake kwa
sasa ni nzuri.
Wakati Ndesamburo akithibitisha kuugua, Katibu wa
Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema jana alilijia juu gazeti hili
akihoji sababu za kuandika habari ya kuumwa kwa Ndesamburo.
Hata
baada ya mwandishi kumweleza katibu huyo Ndesamburo ni kiongozi wa umma
hivyo watu wake wanapaswa kufahamu alipo, bado aliendelea kuhoji kwa
nini iliandikwa akisema habari hiyo ilikuwa na agenda ya kisiasa nyuma
yake.
Ndesamburo hajaonekana katika jukwaa la siasa kwa karibu
mwezi mmoja sasa, hali iliyotafsiriwa ndiyo iliyochochea baadhi ya watu
kuvumisha kuwa hali yake ni mbaya.
Mbunge huyo ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, hakuhudhuria vikao vya Bunge
lililomalizika Ijumaa kutokana na kuwapo kwake nje ya nchi.
Mkurugenzi
wa Idara ya Shughuli za Bunge, John Joel aliliambia gazeti hili jana
kwamba ofisi ya Bunge ina taarifa kuhusu Ndesamburo kwenda kumwona
daktari wake nje ya nchi, kwa ajili ya uangalizi wa kawaida, lakini siyo
kwamba alikuwa mgonjwa sana.
“Ofisi ya Bunge ina taarifa kwamba
Mheshimiwa Ndesamburo alikwenda nje ya nchi kumwona daktari, maana
aliwahi kutibiwa huko na alikuwa ameambiwa kwenda tena huko, kwa hiyo
siyo kwamba yuko mahututi ni uangalizi wa kawaida wa afya yake,” alisema
Joel.
No comments:
Post a Comment