Thursday, November 1, 2012

mwanzo Habari Habari Ulinzi mkali watanda kesi ya Ponda,mbwa,farasi,cctv camera na askari wakutosha.

 
ULINZI wa aina yake uliwekwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu Dar es Salaam jana wakati Katibu  wa  Jumuiya na Taasisi za  Kiislamu Tanzania, Sheikh, Ponda Issa Ponda alipofikishwa mahakamani hapo na watu wengine 49.
Ponda na wafuasi wake walifikishwa mahakamani hapo kusikiliza kesi inayowakabili ,wakidaiwa  kufanya vurugu na kuharibu mali.
Hata hivyo, wakati wafuasi hao wakiachiwa kwa dhamana, Mahakama hiyo ilisema kuwa haina mamlaka ya kisheria ya kutoa dhamana kwa Sheikh Ponda anayetuhumiwa kuchochea vurugu hizo.

Sheikh Ponda na wafuasi wake walifikishwa mahakamani hapo jana asubuhi chini ya ulinzi mkali. Katika viwanja vya Mahakama ya Kisutu pia kulikuwa na ulinzi mkali wa vikosi ya polisi pamoja na kuwekwa vyombo maalumu vya usalama vilivyotumika kuwakagua watu waliokuwa wanaingia hadi Ponda alipoondolewa kurudi rumande baada ya kesi kuahirishwa.
Mbali na wingi wa askari waliokuwa wakilinda usalama katika eneo la mahakama hiyo wakiwa na silaha, mbwa na farasi, pia jana kuliwekwa mashine maalumu ya ukaguzi kwa kila aliyekuwa akiingia mahakamani hapo pamoja na kifaa cha kutambua milipuko.
Mahakamani kulifungwa kamera maalumu za usalama(CCTV) kwenye lango kuu la kuingilia hapo.

Mahakamani
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani na Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi (SSA) Tumaini Kweka ambaye baada ya kesi kutajwa alisema upelelezi wake umeshakamilika na kuiomba  mahakama ipange tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Alisema siku hiyo washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali ya kesi inayowakabili na kutakiwa kubainisha mambo wanayokubaliana nayo na wasiyokubaliana nayo.
Hata hivyo, Wakili wa washtakiwa hao, Juma Nassoro, aliikumbusha mahakama kuhusu dhamana ya washtakiwa hao, akisema walipopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza, maombi yao ya dhamana hayakushughulikiwa kwa vile hakimu aliyepangwa kusikiliza kesi hiyo hakuwapo.
“Mheshimiwa hakimu, kwa kuwa leo upo mwenyewe, basi tunaomba uamuzi wa maombi ya dhamana kwa washtakiwa,”  aliomba Wakili Nassoro.
Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Victoria Nongwa alikubaliana na maombi hayo ya dhamana na kusema kuwa, dhamana iko wazi kwa washtakiwa wote isipokuwa mshtakiwa wa kwanza tu (Sheikh Ponda), ambaye dhamana yake imefungwa na DPP.
“Dhamana iko wazi kwa washtakiwa wa pili hadi wa 50 kwa kuwa makosa yao yanaweza kuwekewa dhamana, isipokuwa mshtakiwa wa kwanza tu, kwa sababu DPP alileta hati ya kuzuia asipewe dhamana,”  alisema Hakimu Nongwa na kuongeza:
“Hivyo mahakama hii haina uwezo wa kisheria kutoa dhamana kwa mshtakiwa wa kwanza mpaka hapo DPP atakapoleta hati nyingine ya kuondoa zuio la awali.”
Kwa washtakiwa wengine, Hakimu Nongwa aliwapa masharti ya dhamana, akiwataka kuwa na wadhamini wawili kwa kila mshtakiwa, wanaotambulika, wenye vitambulisho, na kwamba wote kila mmoja asaini dhamana ya Sh1 milioni.
Pia Hakimu Nongwa aliwaamuru washtakiwa hao wasiende katika eneo la mgogoro uliowasababishia kesi hiyo (Malkazi, Chang’ombe), hadi hapo kesi itakapokwisha.
Baada  ya kutoa masharti hayo ya dhamana, Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 15, kesi hiyo itakaposikilizwa katika hatua ya awali, na kwamba dhamana kwa washtakiwa hao itashughulikiwa kwa taratibu za kawaida kama ilivyo kwa washtakiwa wengine.
Alisema kuwa kila mdhamini anaweza kupeleka mahakamani barua yake ya udhamini wakati wowote, na kama atatimiza masharti hayo ya dhamana, mshtakiwa husika ataachiwa huru kwa dhamana.
Ulinzi mahakamani
Kutokana na kuwapo kwa kesi hiyo, kila mtu aliyekuwa anaingia mahakamani, alikaguliwa kwa kutumia mashine maalumu, huku kamera ikiwa imefungwa lango kuu kuhakikisha kuwa hali ya usalama na amani inatawala kabla, wakati na baada ya kesi hiyo kuisha.
Jumla ya magari saba yakiwa na askari polisi na askari Magereza, zaidi ya 50, waliovalia mavazi maalumu huku wakiwa  na mabomu ya machozi na bunduki, walikuwa wametanda katika eneo lote kuzunguka mahakama.
Pia lilikuwapo gari la maji ya kuwasha,  mbwa watano huku askari wengine wakifanya doria kwa kutumia farasi.
Hata hivyo, kesi hiyo ilisikilizwa mapema sana na kutokana na hali ya ulinzi na ukaguzi mkali uliokuwapo mahakamani hapo, watu wengine waliokuwa na ndugu zao hao waliofikishwa mahakamani hapo, hawakuruhusiwa kuvuka lango la mahakama.
Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, ndugu na jamaa wa washtakiwa hao waliondoka  katika eneo la mahakama kwa makundi, huku askari wakiwasindikiza taratibu hadi walipotokomea.

No comments:

Post a Comment