Sunday, November 11, 2012

Mbowe amtaka Sumaye CHADEMA

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe, amemtaka Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, kuacha kuendelea kulalamikia vitendo vya rushwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na badala yake achukue hatua ya kuvua gamba na kuvaa gwanda.
Mbowe ametoa ushauri huo kwa Sumaye jana wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Katesh wilayani Hanang’ mkoani Manyara katika mkutano wa hadhara kuhamasisha wananchi kupambania haki zao mara baada ya kutoka bungeni mjini Dodoma.
”Nimeshangazwa sana hivi sasa suala la rushwa katika nchi hii kuwa ni kilio cha kila mmoja, hata viongozi wakubwa katika nchi badala ya kuchukua hatua nao wanalia kukithiri kwa vitendo vya rushwa vilivyoota mizizi katika nchi hii, hususani ndani ya chama cha CCM.
“Namshauri Sumaye ambae amekuwa waziri mkuu wa nchi hii kwa miaka 10 na mwaka huu kakumbana na dhoruba kubwa ya kubwagwa katika uchaguzi wa CCM kwa kuzidiwa na nguvu ya rushwa na kubaki kulalamika bila kujua nini anahitajika kufanya.
“Narejea tena kusema kama Sumaye anataka kuidhihirishia nchi hii uadilifu wake, basi ni wakati sasa wa kuionyesha dunia kuwa anakerwa na rushwa kwa kuamua kujiondoa ndani ya CCM na kujiunga na wanamapinduzi wenye lengo la kuikomboa nchi hii kutoka katika lindi la wala rushwa.
”Mwanaume ukiishaangukia pua katika jambo lolote lile, unatakiwa kuamka na kufuta vumbi na kisha kuamua kutoa maamuzi ya nini cha kufanya na kusonga mbele, na sio kulalamika hivyo Sumaye amua moja; Vua Gamba Vaa Gwanda,” alisema Mbowe.
Aidha, katika mkutano huo aliwataka wananchi kufikiria maisha magumu wanayokabiliana nayo hivi sasa, yanayotokana na viongozi waliopo madarakani kuamua kujilimbikizia mali wao na familia zao na kusahau vijana wanaotoka familia masikini.
Alifafanua kuwa kutokana na matabaka kutawala katika nchi hii, ya walionacho na wasionacho hali hiyo imeingia sasa katika sekta ya elimu, ambapo sasa kuna matabaka ya shule za walionacho na wasionacho.
Alisema hali hiyo hivi sasa inaenda kuzalisha watoto wa matajiri na viongozi kuandaliwa kuja kuendelea kuwatawala watoto wanaotoka katika familia za walalahoi, ambao hawawezi kupata elimu bora kutoka katika shule za binafsi zenye kutoa taaluma bora.
Katika mkutano huo, Mbowe alipokea wanachama waliojiengua kutoka CCM na kuamua kujiunga na CHADEMA ambapo aliwataka walioamua kuvua gamba na kuvaa gwanda wawe makamanda wa ukweli ndani ya chama hicho.

No comments:

Post a Comment