Wednesday, November 7, 2012

Balozi wa India aahidi ushirikiano vyombo vya habari

Balozi wa India nchini Debnath Shaw (kushoto), akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando alipotembelea Mkao Makuu ya MCL, Tabata Relini,jijini Dar es Salaam  jana. Picha na Rafael Lubava 

BALOZI wa India nchini, Debnath Shaw ameahidi kuendeleza ushirikiano wa vyombo vya habari kati ya Tanzania na nchi yake kwa muda wote atakaokuwapo hapa nchini.
Aliyasema hayo jana  jijini Dar es Salaam  alipotembelea  Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) na kubadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji  wa Kampuni hiyo, Tido Mhando.
Shaw alisema ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na India atauendeleza  kama ambavyo balozi aliyemaliza muda wake alivyofanya hususan katika sekta ya vyombo vya habari.
Alieleza kuwa katika mkutano wa kimataifa  uliofanyika Novemba 2, mwaka huu  katika Mji wa Gurgaon India uliojulikana  kwa jina la  Indian Ocean Rim, ambao ulihusu ushirikiano wa vyombo vya habari katika Ukanda wa Bahari ya Hindi ulilenga kujadili changamoto mbalimbali za vyombo vya habari na kubadilishana uzoefu.
Katika mkutano huo, nchi 19 za mwambao wa Bahari ya Hindi zilihudhuria huku Tanzania ikiwakilishwa na Mhariri wa Habari za Kimataifa, Andrew Msechu kutoka Gazeti la Mwanachi.
“Nitaendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta ya habari na vyombo vya habari vya Tanzania kwa kuanzisha mafunzo ya kubadilishana uzoefu kwa waandishi,” alisema Shaw.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Tido Mhando  alisema  kampuni yake inahitaji kupata mawasiliano ya karibu na magazeti kutoka India ili kujifunza mambo mbalimbali  yakiwamo ya teknolojia kutoka kwenye magazeti hayo.
“Tunakuomba utusaidie kuimarisha uhusiano  wetu na vyombo vya habari vya  India ili tuweze kupanua zaidi wigo wa habari  hapa kwetu  Tanzania  hasa kwenye upande wa teknolojia “ alisema  Mhando.
Mhando alisema teknolojia ya sasa imekua kwa kiasi kikubwa, hivyo  Kampuni ya Mwananchi Comunications Limited inahitaji kuingia kwenye  mfumo wa digitali ili kuhakikisha inakwenda na wakati.
chanzo-Mwananchi

No comments:

Post a Comment