Wakala wa Juma Kaseja amepeleka maelezo ya mchezaji huyo (CV)
kwa TP Mazembe, lakini akaweka wazi kwamba Simba ndiyo walimharibia kipa
huyo kusajiliwa na klabu za FC Lupopo na Motema Pembe.
Wakala huyo aitwaye Balanga Ismail sasa ni Kocha
wa Sudan Kusini iliyopigwa mabao 2-1 na Zanzibar katika mechi ya awali
ya kombe la Chalenji kwenye Uwanja wa Nyayo.
Balanga aliliambia gazeti hili mjini hapa kwamba,
watu wa Simba ndiyo walimharibia kipa huyo wa Yanga kusajiliwa na klabu
hizo za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Alisema kuwa; “Tulikuwa tumeshamalizana na watu wa
Lupopo, lakini kuna watu wa Simba walipiga simu kwa bosi wa Lupopo
wakamwambia kwamba huyo Kaseja achaneni naye, huwa anauza mechi, yule
bosi akakasirika sana akasema achana naye haraka sana.”
“Nikazungumza na Motema Pembe wakati tunaendelea
kukubaliana mkataba ikatokea hali ileile ya Lupopo, sasa nikashindwa
kuelewa hawa watu wa Simba kwa nini wanamchukia hivi huyu mchezaji? kwa
nini wanamharibia maisha?” alisema Ismail.
“Sasa nimezungumza na watu wa Mazembe na
nimewatumia CV ya Kaseja ndiyo nasikiliza kwenye usajili ujao wanaweza
kumwita, kwa vile wameniambia wanajua uwezo wake,” alisema wakala huyo
aliyesaini miaka miwili kuinoa Sudan Kusini.
Kaseja amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea
Yanga ambayo inashiriki Ligi ya Mabingwa mwakani. Kwa mujibu wa wakala
huyo watu waliokuwa wakipiga simu hizo ni watu wa Simba ingawa hajapewa
majina yao halisi.
No comments:
Post a Comment