Wiki chache zilizopita, kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na mjumbe
mstaafu wa bodi ya wadhamini wa chama hicho kikongwe nchini, Peter
Kisumo, wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere alipata
ujasiri wa ajabu na akatamka sifa za CCM kwa sasa. Kisumo hakusema kwa
siri. Aliweka wazi.
Sifa ya kwanza, amesema CCM ni chama dola, maana huingilia hata
madaraka ya mihimili mingine, huingilia uendeshaji wa Bunge, huingilia
uendeshaji wa mahakama, hivyo hufanya kila liwezekanalo kulazimisha
vitu hata kama sio vya kweli, na havina tija.
Sifa ya pili, CCM inakaa mbali na wananchi. Haya sio maneno yangu, ni
ya Kisumo. Hivyo chama hicho hakipo kwa maslahi ya wananchi wengi hasa
wa hali ya chini. Rejea wimbo wa “Acha waseme Chama Cha Mapinduzi kina
wenyewe”, uliotungwa na Kapteni John Komba.
Sifa ya tatu, imeshindwa kudhibiti rushwa, huduma za jamii nchini
zimedorora, elimu imekuwa mbovu, kila idara inatawaliwa na rushwa.
Watanzania wanajua, Kisumo amesisitiza tu wakielewe chama hiki kuwa
hakiwezi kudhibiti rushwa. Nimeambiwa tumuunge mkono huyu mzee, kuna
kitu tunajifunza hapa.
Sifa ya nne, CCM imeshindwa kuwadhibiti hata walarushwa wenyewe.
Watanzania wanajua, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, na
Mnadhimu wa Upinzani Bungeni walitaja orodha ya mafisadi katika viwanja
vya Mwembeyanga Temeke, lakini hadi sasa CCM imeshindwa kuwadhibiti,
licha ya kututajia kuwa ina mafisadi watatu.
Sifa ya tano, Kisumo amesema CCM ni ya walalamikaji. Hata Rais na
Waziri Mkuu wanalalamika, hawachukui hatua. Watanzania wanajua kuwa
waziri wetu mkuu aliwahi kubanwa kwa kauli zake akaamua kulia bungeni.
Kama Waziri Mkuu analia na kulalamika bila kuchukua hatua zozote,
Watanzania wote wanajua kuwa viongozi wa chama hicho tawala ni
walalamikaji.
Sifa ya sita, amesema CCM ni bubu. Bubu maana yake haiwezi kuongea,
haina sauti, na bubu mara nyingine hasikii, hivyo Kisumo anamaanisha
kuwa chama hicho ni kiziwi, dhana inayoondoa ile nyingine ya kusema ni
sikivu. Bubu hata kama akiwa sikivu hasikii sauti. Hii ni sifa nyingine
ya CCM.
Sifa ya saba, amesema CCM haiwezi kukemea, maana yake ni kama vile
una mbwa ambaye hawezi kubweka, kiziwi, bubu kama inavyobainishwa,
hivyo hana tija hawezi kupambana, ni pambo tu.
Sifa ya nane, amesema CCM ina matumizi mabaya ya rasilimali na
zinatumiwa na wananchi wachache kwa manufaa yao. Hili linajulikana
ndiyo maana viongozi wanalalamika kila mara kuwa pengo kati ya wenye
navyo na wasio navyo linaongezeka. Chama hicho ndio vinara.
Sifa ya tisa, CCM haikubaliki kwa wananchi, hata ikishinda katika
uchaguzi mkuu ujao haitakuwa na nguvu bungeni, itaangushwa. Haya si
maneno yangu ni ya mdhamini wao. Yeye kaona ila najua wengine
wanang’ang’ania kusadikisha watu uongo, kama wanavyofanya Nape, Kinana,
Mangula, Chikawe, Wassira, Lukuvi, Pindi Chana na wengine.
Sifa ya kumi na ya mwisho, CCM kushindwa uchaguzi mkuu ujao uwezekano
ni mkubwa. Huyu kada ameona, ametafakari kwa uzee wake akaona na
akaamua kusema.
Kama huo utabiri ni wa kweli, chama mbadala ni CHADEMA ambacho kinaweza kusaidia wananchi kufanya mabadiliko.
No comments:
Post a Comment