Dar es Salaam. Mwigizaji Bora wa Kike kwa
mujibu wa tuzo za Tamasha la Majahazi la mwaka huu, Elizabeth Michael
maarufu kwa jina la Lulu, amesema anatarajia kuanza kutoa taarifa zote
zinazohusiana na filamu zake kupitia simu za mkononi.
Akizungumza na Mwananchi jana Lulu alisema taarifa
hizo zitapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi hapa nchini.
“Shabiki wangu pia anaweza kuangalia filamu zangu kupitia mitandao ya
kijamii yaani Tigo, Zantel, Vodacom na Airtel. Bado haijawa rasmi hivyo
nitakapozindua ndipo nitakapotoa mwongozo halisi,” alisema Lulu.
Kwa mujibu wa Lulu bado hajajua ni lini bidhaa
yake hiyo itaanza kurushwa hewani ila kwa sasa yupo katika mazungumzo ya
mwisho na wadau wa mitandao ya simu za mikononi.
“Hii ni moja ya mafanikio katika tasnia ya filamu
hivyo siwezi nikasema ni lini mpango huu utaanza kurushwa hewani na
mashabiki kupata huduma hii, ila natarajia kesho (leo) nitaweza kutoa
taarifa rasmi ni lini sasa mashabiki waanze kujiunga na huduma hii.”
Miezi michache iliyopita Lulu alizindua filamu
yake mpya Foolish Age katika ukumbi wa Mlimani City, filamu inayofanya
vizuri sokoni kwa hivi sasa. Hata hivyo Lulu ni kati ya hazina na vipaji
vilivyokuzwa tangu utotoni ambapo anaonyesha kuliteka soko kwa sasa na
huenda anaweza kuwapiku wasanii wakubwa wa kike hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment